Wasomi mnaisaidia vipi jamii?

Mwandishi ni mhitimu wa fani ya Utawala katika Biashara Chuo Kikuu cha Dodoma


Muktasari:

  • Wakati huo sikuwa na matamanio ya kuwa daktari bingwa, mwandishi nguli au mwanasheria aliyebobea kwa sababu niliamini nikifika chuo kikuu nitayafikia matamanio hayo.

Miaka mingi iliyopita wakati ningali mwanafunzi wa shule ya msingi, ndoto yangu kubwa ilikuwa kufikia elimu ya chuo kikuu.

Wakati huo sikuwa na matamanio ya kuwa daktari bingwa, mwandishi nguli au mwanasheria aliyebobea kwa sababu niliamini nikifika chuo kikuu nitayafikia matamanio hayo.

Mwalimu wangu darasani alikuwa akifundisha na kuacha baadhi ya mambo bila kuyafafanua kwa kina kwa maelezo kwamba tukifika chuo kikuu tutaelewa zaidi na hivyo kuniongezea hamasa ya kusoma kwa bidii mpaka daraja hilo.

Nyumbani pia wazazi walinihimiza mara kwa mara kusoma kwa bidii ili nifanikiwe kufika chuo kikuu.

Niliamini (na bado naamini mpaka sasa) kuwa msomi wa chuo kikuu ni mtu mwenye uwezo mkubwa wa kupambanua mambo mbalimbali na kupambana na kila aina ya changamoto katika jamii.

Idadi ya vyuo vikuu ilikuwa ndogo nchini lakini viliweza kutoa mazao bora ya wataalamu katika fani mbalimbali waliopambana na wenzao wa mataifa ya nje na hata kuwapiku. Familia yenye msomi wa chuo kikuu ilikuwa na kila sababu ya kujivunia na kujitapa dhidi ya familia nyingine.

Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni mambo yameanza kubadilika kwa kasi ya kutisha! Idadi ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wanaotamani kufikia kiwango cha elimu ya juu inaporomoka kila kukicha.

Vijana hawa kwa sasa wanatamani kuwa wasanii wa Bongo Fleva na Bongo Movie kuliko wanavyotamani kuwa wahadhiri wa vyuo vikuu.

Utaanzia wapi kumshawishi mtoto wa Kitanzania awe profesa ilhali anawaona vijana wa Bongo Fleva wakichekelea mamilioni kwa onyesho la siku moja?

Utaanzia wapi kumshauri awe mtaalamu wa masuala ya kompyuta na teknolojia kisha aanze kuzurura mtaani kusaka ajira, ilhali anamuona msanii fulani akijikusanyia mamilioni kwa kuchekesha watu?

Lengo la makala haya si kukosoa kazi nzuri zinazofanywa na vijana wenzetu kupitia matumizi sahihi ya vipaji vyao, licha ya wengi wao kutokuwa na elimu kubwa ya vyuo vikuu, bali kujadili sababu ya hawa tunaowaita wasomi kukosa mvuto katika jamii.

Shauku ya familia mbalimbali kuwa na angalau msomi mmoja inazidi kupungua kutokana na wasomi hao kugeuka mizigo katika jamii na tanuru la lawama dhidi ya Serikali, ndugu na jamaa zao.

Msomi huyu aliyesotea elimu kwa zaidi ya muongo mmoja, anategemewa kuwa moto wa kuotea mbali katika kupambana na changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii na kisha kuzibadili kuwa fursa za kujipatia kipato na kuzalisha ajira kwa wengine.

Jamii haitarajii kumuona msomi huyu akilalamikia kukosekana kwa mtaji fedha kama sababu kuu ya kumfanya ashindwe kujiajiri na kuajiri wenzake.

Jamii inaamini msomi ni kama askari aliyepelekwa ughaibuni kupata mafunzo makali ya ukomandoo kwa lengo la kurudi na kupambana na ‘vibaka’ wanaovamia kijijini mara kwa mara na kupora mali zao kwa kutumia silaha za jadi.

Inashangaza kumuona komandoo huyu akiwakimbia vibaka hao kwa maelezo kwamba hawezi kupambana kwa kuwa kijijini hakuna mabomu ya machozi wala silaha nzito za kupambana na vibaka hao!

Muziki wa Tanzania unapendwa na unaongoza kwa kusikilizwa katika nchi zote za Afrika Mashariki! Msomi uliyebobea katika fani ya sheria unaanzia wapi kulalamikia ukosefu wa ajira ilhali wasanii wetu wa Bongo Fleva wanalalamikia kudhulumiwa kazi zao na hata kutapeliwa katika shoo mbalimbali kutokana na kutojua jinsi ya kuingia makubaliano mazuri ya kimikataba?

Hii si ndiyo fursa kwa wasomi hawa kujiajiri badala ya kusubiri ajira kutoka Utumishi?

Tasnia ya filamu Tanzania inaongoza kwa kupendwa katika nchi zote za Afrika Mashariki na Kati! Msomi uliyehitimu shahada ya utawala katika biashara unaanzia wapi kuilalamikia serikali kutokuzalisha ajira ilhali wasanii hawa hawajui mbinu bora za kusambaza kazi zao katika mataifa ya Kenya, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo? Si fursa hii kwa wasomi hawa kuandaa maandiko bora ya miradi ya jinsi ya kuwasaidia wasanii wetu na hatimaye kuwa fursa mpya ya ajira?

Wasomi tuamke, tujitambua na tuwe chachu ya mabadiliko katika jamii ili jamii hiyo ituheshimu. Haisaidii kitu tukiendelea kulalamika na kudhani pengine Serikali itabadili hali ya mambo bila sisi kubadili fikra na mitazamo yetu kuhusu maisha.

Tuache kubweteka vijiweni kwa kuwa msomi ni askari kamili aliyepewa mafunzo muhimu ya jinsi ya kupambana na maadui ujinga, umaskini na maradhi.

Mwandishi ni mhitimu wa fani ya Utawala katika Biashara Chuo Kikuu cha Dodoma