Watanzania milioni tatu kuwa na ugonjwa wa kisukari 2035

Muktasari:

  • Takwimu za sasa nchini Tanzania zinaonyesha kati ya watu wazima 100 takribani watu tisa wana ugonjwa wa kisukari, huku kati ya watu wazima watatu mmoja ana shinikizo la damu.

Ukubwa wa tatizo la Kisukari duniani kote limeendelea kuwa tishio la uhai wa watu mwaka hadi mwaka.

Idadi ya wagonjwa wa Kisukari kama yalivyo magonjwa mengine yasiyo ya kuambukizwa ikiwemo yale ya moyo na shinikizo la damu, figo, magonjwa ya mfumo wa hewa na saratani, yanazidi kuongezeka kwa kasi na yanaendelea kuwa chanzo kikuu cha vifo duniani kote.

Inakadiriwa kisukari pekee kimeathiri maisha ya watu takribani milioni 425 duniani kote hadi mwaka 2017 huku asilimia 80 ya idadi hiyo ikiwa ni katika nchi za kipato cha chini ikiwamo Tanzania.

Wataalamu wanaonya kuwa ongezeko la wagonjwa wa Kisukari ni la kasi ukilinganisha na ongezeko la idadi ya watu duniani, kufuatia takwimu zinazoongezeka kwa kadri miaka inavyosonga.

Mwaka 1985 dunia nzima ilikuwa na watu bilioni 4.85 ambapo watu milioni 30 walikuwa na kisukari.

Mwaka 2017 dunia ilikuwa na watu bilioni 7.55, na watu milioni 425 walikuwa na kisukari.

Takwimu zilizotolewa mapema wiki hii na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Profesa Lawrence Museru wakati wa maadhimisho ya siku ya Kisukari duniani takwimu zimeonyesha kuongezeka kwa watu wenye Kisukari nchini.

Anasema kufuatia ukubwa wa tatizo hilo, kliniki ya kisukari katika Hospitali ya Taifa Muhimbili inawahudumia wagonjwa zaidi ya 6000 kwa mwaka.

“Kama kasi hii ikiendelea hivi, Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa kufikia mwaka 2035 idadi ya wagonjwa wa Kisukari duniani itafikia watu milioni 592 na Tanzania itakuwa na wagonjwa zaidi ya milioni 3,” anasema.

Profesa anasema takwimu za sasa nchini Tanzania zinaonyesha kati ya watu wazima 100 takribani watu tisa wana ugonjwa wa kisukari, huku kati ya watu wazima watatu mmoja ana shinikizo la damu.

Katika utafiti wa STEPS uliofanywa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Taasisi ya utafiti wa mgonjwa ya binadamu (NIMR), na Shirika la Afya Duniani, mwaka 2012 uliohusisha wilaya 50 nchini Tanzania, ulionesha kuwa asilimia 9.1 ya Watanzania wenye umri kati ya miaka 25 hadi 64 wana ugonjwa wa kisukari.

Hiyo ilimaanisha kuwa, katika kila watu 11 nchini mtu mmoja ana kisukari.

Daktari bingwa wa magonjwa ya kisukari Elisante Banduka anashauri kila mtu kupima mara kwa mara ili kuyagundua magonjwa mapema.

Anasema gharama ya kukabiliana na magonjwa hayo ni mabilioni ya shilingi ambayo si Serikali wala wananchi wataweza kuyahimili.

“Jitihada za kukabiliana na tatizo hili hazina budi kujikita zaidi katika mitazamo jumuishi inayolenga kukinga ili kupunguza kiwango cha magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo Kisukari,” anasema.

Mwenyekiti wa chama cha ugonjwa wa kisukari na muungano wa vyama vya magonjwa yasiyoambukiza Profesa Andrew Swai, anasema katika magonjwa yasiyoambukiza ambayo ni moyo, saratani, kisukari na magonjwa sugu ya mapafu yanachangia asilimia 30 ya vifo.

Akizungumzia zaidi kuhusu ugonjwa wa kisukari, Profesa Swai anasema ili binadamu aishi anatakiwa kula chakula ili apate nguvu na aweze kupumua.

Hilo ni zoezi la tangu kuzaliwa hivyo lazima sukari ipatikane mwilini ili ubongo, maini, figo, mapafu viweze kufanya kazi, lakini anaonya kwamba vikizidi huleta madhara.

“Unapokula sukari ikaingia tumboni inakutana na hewa na kutengeneza nguvu, sasa sukari inatakiwa kuja kidogokidogo kadri inavyohitajika, mfano ukichoma nyama ukazidisha moto nyama inaungua na mwilini mwako ile nguvu kutokana na sukari na hewa vinapoungana ikizidi ile nguvu ya ziada itachoma mwili, ndiyo maana wenye kisukari wanapofuka macho, mishipa ya fahamu, figo, mishipa ya damu,” anasema.

Kauli ya Wizara

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu anasema kuwa katika kudhibiti ugonjwa wa kisukari, Wizara yake inatekeleza mkakati wa Taifa wa kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza wa mwaka 2016 - 2020 ambapo ugonjwa wa Kisukari ni moja ya magonjwa yanayolengwa.

Anasema maeneo ya kipaumbele ya kudhibiti ugonjwa wa kisukari nchini ni pamoja na kukinga, kuimarisha huduma za upimaji kwa ajili ya ugunduzi wa mapema na kutibu.

“Hivi sasa watoto wote na vijana chini ya miaka 22 walio na Kisukari wanapata mahitaji yao yote ya matibabu bure kupitia kliniki za kisukari zilizopo nchini. Lengo letu ni kupunguza wagonjwa wa kisukari kwa asilimia 28 ifikapo 2025,” anasema.

Anasema sambamba na kuhamasisha wananchi kujikinga na ugonjwa wa kisukari, lengo la Serikali ni kuhakikisha inapanua huduma za kupima na matibabu kwa wagonjwa wa kisukari kwa kuimarisha kliniki za kwa vituo vyote vya afya nchini ikiwemo kutoa mafunzo kwa madaktari na wauguzi.