Watanzania tujenge utamaduni wa kujisomea

Muktasari:

Matokeo yake sasa licha ya elimu kuonekana kukua bado watu wengi hawana maarifa. Ni kweli idadi ya shule imeongezeka, lakini shule hizi hazijasaidia kuweka utamaduni wa watu kusoma vitabu.

Kama kuna tatizo linalotukabili Watanzania katika maendeleo ya sekta ya elimu, basi ni kukosa utamaduni wa kusoma vitabu, majarida na machapisho.

Matokeo yake sasa licha ya elimu kuonekana kukua bado watu wengi hawana maarifa. Ni kweli idadi ya shule imeongezeka, lakini shule hizi hazijasaidia kuweka utamaduni wa watu kusoma vitabu.

Wanafunzi wengi iwe ni shule za msingi, sekondari au vyuo hawako tayari kujisomea vitabu. Ukiona mtu anasoma kitabu basi anataka kujibu mitihani na kwa kuwa elimu yetu imekuwa ni ya kujibu mitihani basi hata wasomi wengi hawana maarifa, siyo wabunifu na watatuzi wa kero katika jamii.

Ukitaka kujua kuwa hatuna utamaduni wa kusoma, angalia hata idadi ya magazeti yanayouzwa mitaani. Ukilinganisha na nchi nyingine, Tanzania ina wasomaji wachache mno wa magazeti na majarida.

Kwa mfano, nchi ya Kenya, magazeti yanayoongoza kwa mauzo huuza hadi nakala 200,000 kwa siku tena ni ya lugha ya Kiingereza, wakati kwa Tanzania magazeti yanayoongoza kwa mauzo ni ya Kiswahili, lakini ni machache mno yanayoweza kuuza angalau nakala 50,000.

Yanayofika idadi hiyo au zaidi, usishangae kuona ni yale ya michezo na udaku. Na haya ni kwa sababu yana habari fupi fupi na za kuburudisha zaidi, si za kuchimba mambo makini kwa undani.

Hata Wabunge wetu wengi hawasomi. Hawasomi vitabu, hawasomi ripoti na mikataba mbalimbali, ndiyo maana hata michango yao imejaa ushabiki tu wa vyama vyao, badala ya kujikita kwenye hoja za msingi.

Kwa kuwa hatusomi vya kutosha, hatuna maarifa kama wenzetu na ndiyo maana wanatumia fursa nyingi za maendeleo zilizopo nchini kwetu.

Tuna bahati mbaya Watanzania kwa sababu watu wengi hawaamini kwenye kujibidiisha kikazi bali wengi wanaamini kupitia njia za mkato.

Hata maneno na misamiati ndiyo kama hiyo ya ‘Voda fasta’, ‘jirushe’, mini kabang’ na mingineyo. Ni misemo itokanayo na promosheni za mitandao ya simu, lakini inaakisi maisha halisi ya Watanzania, kwamba tunapenda maisha ya mteremko sana.

Wanafunzi wengi hawasomi vitabu, hata wanaosoma kujibia mitihani hawasomi vya kutosha ndiyo maana matokeo ya mitihani ni mabaya kila mwaka.

Halafu wahitimu wa vyuo vyetu wakifika kwenye usaili wa ajira hawawezi kujieleza, achilia mbali kwa Kiingereza, hata kwa Kiswahili. Wengi hawajiamini, kwa sababu hawasomi barabara.

Wataalamu wa afya ya akili wanaamini kuwa ubongo wa binadamu ni kama shamba tupu linalohitaji kupandwa maarifa. Mtu anapojibidiisha kusoma huujaza ubongo maarifa ya kupambana na mazingira yake.

Tabia ya kujisomea hujengwa, haiji hivi hivi tu. Tatizo ni kwamba hata walimu wetu si wasomaji wa vitabu ndiyo maana wanashindwa kuwaambukiza wanafunzi.

Walimu wenyewe wengi walifeli mitihani, wamepata daraja la nne. Kwa hali hii kweli watamhimiza mwanafunzi kusoma vitabu.

Tabia ya kusoma vitabu, majarida na mitandao ya maarifa, kama vile Wikipedia, inapaswa kupandwa tangu watoto wakiwa kwenye elimu ya awali. Watoto wafundishwe kusoma vitabu.

Kwa mfano, Serikali kwa kushirikiana na wadau, wajenge maktaba kuanzia shule za awali, msingi, sekondari na vyuo.

Mtu asipewe kibali cha kuanzisha shule hata ya awali kama hajajenga maktaba japo rahisi tu. Watoto wafundishwe umuhimu wa kusoma vitabu, magazeti na majarida. Walimu wawapangie wanafunzi idadi ya vitabu vya kusoma kwa lazima.

Ni kweli tunazo maktaba kwa kila mkoa zinazosimamiwa na Bodi ya Huduma za Maktaba (Bohumata), lakini shirika hili linapaswa kwenda mbali zaidi kwa kuweka maktaba kwa kila kata na si wilaya tu.

Hiyo itawawezesha wanafunzi wengi walioko vijijini kujisomea vitabu na magazeti hivyo wataerevuka kila siku na kukuza ufahamu wao.

Watu wakijisomea kwa wingi wataweza kujenga hoja na kuchukua hatua kila inapobidi. Taifa la watu wanaosoma sana huchangamka kwa mijadala. Watu wake huwa na ujasiri wa kuhoji mambo pale wanapoona hapaendi sawa.

Leo Tanzania ni nchi masikini licha ya kuwa na rasilimali nyingi, lakini Watanzania wengi wanaonekana kuridhika kwa kuwa hawajui kinachoendelea. Hawajui kwa sababu hawasomi. Kama watu wangesoma wasingeridhika na hali iliyopo.

Tutofautishe kusoma na kujisomea. Mtu anaweza kuwa amesoma hadi chuo kikuu, lakini hana tabia ya kujisomea vitabu, majarida, mitandao ya maarifa na machapisho.

Tukijenga tabia ya kujisomea tutajikomboa kifikra na kuikomboa nchi yetu.

Elias Msuya ni mwandishi wa Mwananchi. 0754 897 287