Watendaji wa chini nao hawamwelewi Rais Magufuli

Muktasari:

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo wakati wa hafla fupi ya kumuapisha Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam. Chanzo cha kauli hiyo ni baada ya kutoridhishwa kwake na utendaji kazi wa viongozi wa Wizara ya Madini.

Hivi karibuni, Rais John Magufuli alitamka wazi kwamba baadhi ya wateule wake, bado hawajamuelewa anataka nini katika Serikali yake ya awamu ya tano.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo wakati wa hafla fupi ya kumuapisha Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam. Chanzo cha kauli hiyo ni baada ya kutoridhishwa kwake na utendaji kazi wa viongozi wa Wizara ya Madini.

Alitoa mifano kadhaa ya mambo yanayosuasua kwenye wizara hiyo na kuwataka wahusika kubadilika haraka.

Kana kwamba haitoshi, Rais pia aliunyooshea kidole utendaji usioridhisha wa Wizara ya Kilimo katika suala la kusimamia usambazaji wa mbolea nchini.

Ni wazi tangu aanze kazi ya urais wa nchi yetu, Magufuli ameweka wazi dhamira yake ya kulitumikia Taifa kwa uaminifu na uadilifu wa hali ya juu, huku akiwataka wateule wake na wafanyakazi wa umma kuhakikisha wanaondoa kero kwa wananchi.

Amekuwa akisema katika Serikali yake hataki rushwa, lakini wapo wafanyakazi wa umma ambao wanaona bila rushwa hawatafanikiwa. Kwa mfano, madereva wa malori na mabasi bado wanalalamikia rushwa kutoka kwa polisi wa usalama barabarani.

Utendaji kazi wa askari hao wa kusimamisha magari na kufuatwa na makondakta kwa mbali bila ya wao kukagua makosa ya magari, kunaashiria kuwapo kwa tabia ya rushwa.

Hali kadhalika makarani wa mahakama, sasa wanatajwa kuwa ni madalali au watu wa kati kwa kuchochea walalamikaji au walalamikiwa watoe rushwa ili kesi zao zimalizwe vizuri.

Makarani wa mahakama wanadaiwa kuwataka wenye kesi watoe fedha kwao ili wakawasilishe kwa mahakimu wanaosikiliza kesi zao.

Bila shaka watumishi wanaotenda hayo ni wale wasioielewa Serikali ya Awamu ya Tano kwamba haitaki kero za aina hiyo.

Serikali hii pia ilitamka wazi kila mtu afanye kazi na ni marufuku kunywa pombe, kucheza bao na ‘pool’ asubuhi. Ni kweli mwaka 2016 ulikuwa mwaka wa vita dhidi ya ulevi, dawa za kulevya na uzururaji. Viongozi wa ngazi ya kitaifa, mikoa hadi wilaya walichachamaa.

Lakini cha ajabu taarifa za kukamatwa kwa dawa za kulevya hususan bangi mitaani katika miji mingi kwa sasa zimepoa wakati wavutaji wapo.

Kana kwamba haitoshi, navyo vilabu vya pombe za kienyeji, mabaa yameanza tena kufunguliwa asubuhi. Michezo ya bao na ‘pool’ asubuhi imerudi kuanzia mijini hadi vijjini.

Mambo hayo yanafanyika wakati Wakurugenzi wa halmashauri wapo, watendaji wa mitaa na vijiji wapo na vyombo vya dola vyote vipo. Bila shaka yanafanyika kwa sababu ya kutomuelewa Rais na Serikali yake.

Serikali ya awamu hii ilishatamka elimu bure kwa wanafunzi wa darasa la kwanza hadi kidato cha nne, lakini cha ajabu, bado wananchi wanalalamika kwamba wanatakiwa kulipa fedha kwanza ili kuandikisha watoto wa darasa la kwanza.

Vitendo hivi vinafanyika kwa sababu viongozi wa halmashauri hadi kwenye shule husika hawajaielewa Serikali ya awamu ya tano inataka nini. Hali hii imemlazimisha Rais Magufulu kurudia kutoa onyo kali kwa wahusika. Lakini wapo wanaohoji ni kwa vipi watoto watasoma bila chakula cha mchana.

Bila shaka wanaohoji ni wale wagumu wa kuelewa mambo. Je, hawawezi kuwashauri watoto walete vyakula kutoka nyumbani?

Pia wapo walimu wanaowarudisha wanafunzi nyumbani wakiwataka wakawaite wazazi wao ambao wanadaiwa hawakutoa michango ya majengo.

Kimsingi, suala la michango ya majengo au maendeleo yoyote kutoka kwa wazazi iendelee, lakini mwanafunzi asihusishwe na kukatishwa masomo.

Naamini ni busara zaidi kuwaita wazazi wanaokaidi maendeleo kwa kutumia mgambo kuliko kuwatuma wanafunzi. Suala la ujenzi wa shule liendelee bila ya kuwabughudhi watoto.

Serikali ya Rais Magufuli pia ilishatoa tamko kwamba maofisa ugani wawafikie wakulima na wafugaji ili kuwaelimisha kufanya shughuli zao kitalaamu, lakini msimu wa kilimo huu, wakulima wanahangaika peke yao. Ndiyo maana hawakutoa taarifa mapema za umuhimu wa kuwahisha mbolea maeneo mbalimbali nchini.

Bila shaka, watumishi wa umma lazima watambue kwamba Rais anawataka wawe mfano mzuri kwa Watanzania na watekeleze vizuri majukumu yao.

Hata hivyo, ipo haja ya kuzipongeza baadhi ya ofisi au taasisi za umma ambazo zinafanya kazi kwa nia nzuri yenye mabadiliko licha ya kukabiliwa na uhaba wa vitendea kazi.

Kwa mfano, taasisi za afya zimeonyesha mabadiliko ya kuelekea kwenye utendaji mzuri, licha ya kuwapo kwa watumishi wachache wenye vichwa vigumu.

Lauden Mwambona ni mdau wa maendeleo anayeishi mkoani Mbeya