Watoto na tishio la kupata maradhi yasiyo ya kuambukiza

Miaka ya zamani ilikuwa kawaida kuona wanafunzi wakikimbia mchakamchaka huku wakiimba nyimbo za kusifia, kukosoa, kujenga uzalendo na hata zile zilizokuwa zikimpinga Nduli Idd Amini.

Wapo waliodhani mchakamchaka ni kwa ajili ya kujifurahisha tu kumbe lah! Wanafunzi walikimbia ili kuimarisha afya zao na kujikinga na maradhi yasiyo ya kuambukiza.

Siku hizi hali imebadilika. Shule nyingi wanafunzi wake hawakimbii mchakamchaka wala hawafanyi mazoezi.

Mratibu wa maradhi yasiyo ya kuambukiza Mkoani Dar es Salaam, Dk Digna Riwa anasema aina ya maisha ya watoto wanayoishi siku hizi inawaweka kwenye hatari kubwa ya kupata maradhi yasiyoambukiza.

Akizungumza katika uzinduzi wa mchakamchaka shuleni, uliofanyika katika Manispaa ya Ilala hivi karibuni, Dk Riwa anasema watoto wengi wanakosa muda wa kufanya mazoezi huku wakipatiwa vyakula vya mafuta, jambo linaloendelea kuhatarisha maisha yao.

“Lipo tishio kubwa kwa watoto kupata maradhi yasiyo ya kuambukizwa hasa ya moyo na pumu kwa sababu, hawana mazoezi ya afya,” anasema.

Watoto wengi wakiamka asubuhi hukutana na usafiri wa kuwapeleka shuleni, na kurejeshwa nyumbani, wanafungiwa huku wakila vyakula vingi vya mafuta hii ni hatari,” anasema daktari huyo.

Maradhi yasiyo ya kuambukiza ni yale ambayo hayasambai kwa mtu yeyote kwa kuwa hayana vimelea vinavyohusiana na maradhi hayo.

Maradhi hayo ni pamoja na kisukari, shinikizo la damu, athma (Pumu) na saratani.

Dk Riwa anasema ugonjwa wa pumu na moyo ni tishio zaidi kwa watoto.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Kiraia ya Kinga dhidi ya Magonjwa (CCP-Madicine Medical Centre), Dk Frank Manase, anasema maradhi hayo yamekuwa chanzo kikubwa cha maumivi ya mwili, akili na kiroho kwa familia nyingi za Kitanzania.

“Kitendo cha kupoteza kiungo kimoja mfano mguu au jicho wakati bado unayahitaji, yaweza kuleta mateso yasiyovumilika kwa mtu yeyote,” anasema.

Anasema zipo familia nyingi zimeporomoka kiuchumi kwa sababu ya kuwa na mmoja wa wanafamilia mwenye moja ya maradhi sugu.

Kwa nini mchakamchaka kwa wanafunzi

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Nito Pallera anasema shule nyingi hazina utaratibu wa wanafunzi kukimbia mchaka mchaka jambo ambalo ni hatari kwa afya za watoto.

Dk Manasema anasema miezi sita iliyopita waliweka kambi ya upimaji afya wakitizama hasa maradhi ya moyo, seli mundu (sickle cell disease) afya ya akili, kinywa na meno, pua, koo na masikio.

Anasema matokeo waliyokutana nayo yaliwatisha kiasi cha kufikiria nini cha kufanya ili kuwasaidia watoto.

Walibaini wengi wao wanasumbuliwa na maradhi ya athma, moyo na mengine kwa sababu ya kutopimwa afya zao wala kufanya mazoezi.

“Kwetu sisi tafsiri ya mchakamchaka siyo michezo kama wengine wangesema, bali ni njia ya kupima afya, kutoa kinga ya afya na pia ni tiba kwa maradhi,” anasema Dk Manase.

Anasema kiuhalisia mtoto mwenye matatizo ya moyo, sickle cell, au pumu akiambiwa akimbie mchakamchaka na wenzake hataweza kumaliza nao kwa wakati mmoja.

Kwani atataka apumzike mara nyingi njiani na hataweza kumaliza kwa wakati kama wenzake.

“Hivyo kuna uhitaji wa kambi ya upimaji afya ili kuwabaini hawa watoto wenye maradhi, hivyo kupitia mchakamchaka, itakuwa kipimo tosha cha afya kwa upande mmoja,” anasema.

Anasema maradhi yasiyoambukiza huweza kusababisha vifo vya ghafla na mtoto mwenye pumu asipopata huduma ya haraka na sahihi, anaweza kupoteza maisha ndani ya dakika chache.

“Hivyo kumtambua mtoto mwenye pumu ni muhimu sana kuliko hata kuwa na wodi ya kumlaza inapombana,” anasema Dk Manase.

Hali ya maradhi kwa watoto

Wataalamu wa afya wanasema kutokana na hali ya maisha kubadilika na watu kubadili mienendo ya maisha kwa kula vyakula vya kisasa, vingi vikiwa ni vile vinavyozalishwa viwandani, maradhi yasiyo ya kuambukiza yameanza kubisha hodi kwa kasi kubwa kwa watoto na vijana.

Takwimu zilizotolewa na Baraza la Afya Duniani kupitia Mzunguko wa Malengo ya Lishe (2025), zinaonyesha katika kila watoto 25 walio chini ya umri wa miaka mitano Tanzania, watano kati yao wanakabiliwa na tatizo la uzito uliozidi kiasi jambo ambalo ni hatari.

Pia, takwimu za kituo cha maradhi ya kudhibiti uzito nchini Marekani zinaonyesha kati ya watoto watano, mmoja anauzito uliokithili au mkubwa.

Kwa mujibu wa Jarida la tiba la Uingereza, ‘The Lancet’, Volume 387, la Aprili 2, 2016, vifo vinavyotokana na kunenepa kupita kiasi ni mara tatu zaidi ya vifo vinavyosababishwa na kukosa chakula chenye lishe, ingawa bado nchi nyingi zinapambana na ukosefu wa chakula.

Wataalamu hao wanasema unene huyo ndiyo unawaweka watoto kwenye hatari ya kupata maradhi yasiyo ya kuambukiza.

Hali hiyo inawaweka katika hatari zaidi ya kupata maradhi hayo wakati wa kubalehe na ujana wao.

Wataalamu wa lishe kutoka Jukwaa la Lishe nchini (Panita), wanasema unene kupita kiasi ni ugonjwa wa utapiamlo utokanao na kula kupita kiasi.

Wataalamu hao wanasema matajiri na watu wenye kipato cha juu nchini ndiyo walio kwenye hatari kubwa zaidi ya kukumbwa na ugonjwa huo kutokana na kula vyakula vya gharama na visivyo na tija kwenye mwili.

“Kunenepa kupita kiasi maana yake ni mtu kuwa na uzito uliozidi wakati uzito wa mwili wake unakuwa mkubwa ukilinganishwa na mwili wake, huu ndiyo utapiamlo,” anasema Ofisa wa Panita, Lucy Maziku.

Maziku anasema utafiti unaonyesha matukio ya watu kunenepa kupita kiasi yanaongezeka jambo linaloongeza ukuaji wa tatizo la utapiamlo, sio tu kwa maradhi nyemelezi.

Hatua zinazochukuliwa

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Pallera anasema atasimama kuhakikisha wanafunzi wa manispaa hiyo wanatengewa muda wa kukimbia mchakamchaka kama njia ya kupambana na maradhi hayo.

Anasema hakuna ubishi kwamba njia pekee itakayowawezesha kutimiza malengo yao ni afya njema inayotokana na ufanyaji wa mazoezi, lishe bora na elimu nzuri.

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, anakiri kuwapo kwa tishio hilo na kuwataka wazazi kushiriki kuhakikisha watoto wao wanakuwa na afya bora kwa kuwafanyisha mazoezi badala ya kuwafungia ndani, huku wakitumia magari kwenda na kurudi shule.

Wanafunzi walonga ugumu wa mchakato

Hata hivyo, baadhi ya wanafunzi walisema itakuwa vigumu kwao kufanya mazoezi kutokana na baadhi ya shule kukosa maeneo ya michezo.

Ofisa Elimu, Ofisi ya Kamishna wa Elimu, Kenneth Konga anasema ipo haja kwa shule zote kuhakikisha zinatenga maeneo ya wazi kwaajili ya michezo kama sera inavyotaka.

Anasema changamoto pekee inayozikaba shule hizo ni kutokuwapo kwa maeneo hayo jambo ambalo linahatarisha afya za watoto.