Watu waelimishwe umuhimu wa kupima afya

Muktasari:

  • Kwamba “Mungu akituwezesha katika mkoa wetu,” Makonda anasema “tupite kila nyumba kupima tezi dume na tutapata wataalamu wa kutosha. Nina uhakika na kampeni hii tukishamaliza hii ya kuchanja watoto wa miaka 14, tutahakikisha tunapita kila nyumba”.

Wiki iliyopita Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alipitisha uamuzi ambao ulipokewa kwa hisia tofauti kuhusu suala la kupima afya ili kutambua mapema na kutibu saratani ya tezi dume.

Kwamba “Mungu akituwezesha katika mkoa wetu,” Makonda anasema “tupite kila nyumba kupima tezi dume na tutapata wataalamu wa kutosha. Nina uhakika na kampeni hii tukishamaliza hii ya kuchanja watoto wa miaka 14, tutahakikisha tunapita kila nyumba”.

Alizungumza hayo wakati akifungua warsha ya chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi (HPV) kwa wasichana wa miaka 14 iliyovishirikisha vyombo vya habari, wataalamu wa afya na viongozi mbalimbali wa dini na siasa. Alisema watu wengi hugundulika kuwa na ugonjwa huo katika hatua za mwisho ambazo husababisha kifo.

Saratani ya tezi dume huathiri tezi iliyo katika mfumo wa uzazi wa mwanaume ambayo ipo chini ya kibofu cha mkojo na kuzunguka sehemu ya juu ya mirija inayosafirisha mkojo kwenda kwenye kibofu. Tezi hiyo ndiyo huzalisha majimaji yanayorutubisha na kusafirisha mbegu za kiume.

Tunaielewa nia njema ya mkuu wa mkoa. Tunatambua shauku yake kutaka kuongoza wakazi wenye afya njema, wanaojishughulisha na kazi za kujenga Taifa, lakini tunashauri kuwa elimu ya kutosha inatakiwa kutolewa kwa watu kabla ya kuanza kwa upimaji huo.

Tunasisitiza suala hilo la elimu baada ya kutokea mjadala mkubwa miongoni mwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam huku wengine wakidhani suala hilo ni lazima, wengine wakionekana kutoelewa kinachoendelea na kundi jingine likipinga tu.

Elimu ikitolewa watu wengi watajitokeza na kutoa ushirikiano. Mfano, chini ya usimamizi wake, kwa miaka miwili mfululizo iliandaliwa kliniki kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja kupima presha, moyo na kisukari siyo saratani ya tezi dume. Watu walijitokeza kwa sababu kuna elimu iliyokuwa imetolewa kwanza.

Watanzania wote wana kumbukumbu nzuri ya namna Rais Jakaya Kikwete alivyoanzisha kampeni kwa wanaume kupima saratani ya tezi dume mwishoni mwa awamu yake ya pili.

Alielezea namna ugonjwa huo ulivyo na ulivyomsumbua hadi alipoamua kwenda kutibiwa Marekani, na kwa hekima baada ya kurejea nchini alitoa wito wanaume wasiogope kupima.

Kikwete alitumia muda mrefu kwenye Televisheni ya Taifa kutoa elimu kupitia hotuba yake alipofika Uwanja wa Ndege na lengo kubwa alitaka wanaume waujue ugonjwa huo, madhara yake ili waone umuhimu wa kupima na kutibu.

Elimu kama hiyo inapaswa kufanywa kupitia maeneo mbalimbali kuanzia kwenye vyombo vya habari, sehemu za kazi katika makundi tofauti na hata katika jamii yote kwa ujumla. Uzoefu wetu ni kwamba kila inapofanyika kampeni ya kupima magonjwa fulani, viongozi wetu huwa wanatoa takwimu kuonyesha jinsi ugonjwa fulani unavyoongoza kwa vifo.

Magonjwa tofauti hutajwa kuwa yanaongoza kwa vifo kwa kuangalia eneo fulani, kama vile saratani kuongoza kwa vifo kwa magonjwa yasiyoambukiza au saratani ya kizazi kuongoza kwa kuua kwa magonjwa ya saratini. Wataalamu wanasema magonjwa yasiyoambukiza husababishwa kwa kiasi kikubwa na mtindo wa maisha na hupendekeza watu wabadili aina ya vyakula, kufanya mazoezi na kupima afya.

Sisi tunaamini kuwa afya ni jambo muhimu sana katika jamii na tungependa kampeni za namna hii ziwe zinafanyika mara kwa mara, lakini suala la elimu linapaswa kupewa kipuambele zaidi ili wahusika wajue baada ya kupima, utaratibu gani utatumika kwa ajili ya matibabu.