Uokoaji wa helikopta waanza Mlima Kilimanjaro

Muktasari:

  • Taarifa iliyotolewa jana na ofisa mawasiliano wa kampuni hiyo, Rashid Mhina inasema waokoaji wana uwezo wa kufika eneo la dharura ndani ya dakika tano tangu kupokelewa kwa simu.

Moshi. Kampuni ya Kilimanjaro SAR Limited imeanza rasmi kutoa huduma za utafutaji na uokoaji wa watalii wanaopanda mlima Kilimanjaro na Meru, kwa kutumia helikopta yenye vifaa vya kisasa.

Taarifa iliyotolewa jana na ofisa mawasiliano wa kampuni hiyo, Rashid Mhina inasema waokoaji wana uwezo wa kufika eneo la dharura ndani ya dakika tano tangu kupokelewa kwa simu.

Huduma hiyo imekuja kipindi ambacho kumekuwa na kilio cha muda mrefu cha watalii na waongoza watalii (Guides), kuhusu uduni wa vifaa vya uokoaji katika hifadhi ya Mlima Kilimanjaro.

“Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya watalii 45,000 hutamani kupanda kilele cha mlima huo mrefu Afrika, kwa bahati mbaya usalama wa maisha yao imekuwa kizuizi kwao kutimiza ndoto hiyo,” alisema Mhina.

Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa) ilianzishwa mwaka 1973 na kufunguliwa rasmi kwa ajili ya utalii mwaka 1977.

Mhifadhi mkuu wa zamani wa Kinapa, Erastus Lufungulo alikaririwa akisema kwamba watalii 56,000; wapagazi na waongozaji 168,000 hupanda mlima huo kila mwaka hivyo kufanya jumla yake kufikia 224,000.

Lufungulo alisema kwamba takwimu za uokoaji za Kitengo cha Uokoaji Kinapa zinaonyesha kuwa asilimia 20 ya wapandaji sawa na wapandaji 44,800, wamekuwa wakikumbwa na magonjwa ya mlimani.

Alisema uokoaji wa helikopta ulikuwa ikihitaji kuhakikisha usalama wa watalii unakuwa wa uhakika zaidi.