Thursday, November 2, 2017

Gharama za uendeshaji zaikaanga benki ya kilimo

“Hawa watu uliwaleta kwa gharama kubwa mwaka

“Hawa watu uliwaleta kwa gharama kubwa mwaka jana na wakaondoka ukawalipa gratuity ya Sh300 milioni...labda unieleze ukijumlisha miaka miwili unafika Sh500 milioni kwa benki changa bado napata shida.”Ezekiel Maige 

By Sharon Sauwa, Mwananchi ssauwa@mwananchi.co.tz

Dodoma. Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imeiagiza bodi ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kuhakikisha gharama za uendeshaji ikiwamo mishahara, mikopo na kodi za pango zinapungua.

PAC ilitoa agizo hilo juzi baada ya kupitia hesabu za benki hiyo za mwaka wa fedha 2015/16, zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Akitoa maagizo hayo juzi, mwenyekiti wa kamati hiyo, Naghenjwa Kaboyoka alisema benki hiyo ni taasisi changa lakini gharama za uendeshaji ziko juu.

“Hasa mishahara, mikopo mingine ya watumishi hivyo kamati inaiagiza bodi kuhakikisha gharama hizi zinapungua,” alisema.

Kaboyoka ambaye pia ni mbunge wa Same Mashariki, alisema agizo jingine ni benki kuangalia upya gharama za pango ili kuona kama wanaweza kutumia sehemu ya jengo hilo au kutumia majengo ya Serikali kwa sababu ofisi nyingi za Serikali zimehamia Dodoma. Pia, iliiagiza bodi hiyo kujenga majengo yake kwa kutumia mashirika yanayojenga kwa gharama nafuu.

Kaboyoka aliagiza bodi hiyo kuwasilisha kwa CAG mkataba, mchanganuo na gharama kuhusu mfumo wa Tehama (software) na leseni baada ya kamati kushindwa kupata majibu ya kuridhisha.

Baadhi ya wabunge waliochangia akiwamo, Ezekiel Maige wa Msalala alisema katika vitabu vyao mafao (gratuity) ilikuwa Sh221 milioni lakini imepanda hadi Sh265 milioni.

Mbunge wa Magomeni, Jamal Kassim alisema katika vitabu inaonekana uamuzi wa kununua mfumo wa Tehama haukufanywa na benki hiyo, bali ofisi ya waziri mkuu.

Naye mwenyekiti wa bodi ya TADB, Rosebud Kurwijila alisema wataangalia suala la kuajiri ili kupunguza gharama zinazotokana na kuajiri mpya.

Kuhusu ununuzi wa Tehama, kaimu mkurugenzi mtendaji wa benki hiyo, Francis Assenga alisema fedha za kufunga mfumo huo zilipatikana kupitia mradi wa PSP ambao upo chini ya ofisi ya waziri.

-->