Sh150 milioni za Benki ya Posta zatumika kuhudumia jamii

Muktasari:

  • Alisema fedha hizo zimetumika kujenga madarasa, zahanati, matundu ya vyoo, kununua madawati, mashuka na vitanda katika hospitali mbalimbali.

 Benki ya Posta Tanzania (TPB) imetumia Sh150 milioni mwaka huu kusaidia shughuli za kijamii katika mikoa inayotoa huduma za kibenki.

Meneja Mawasiliano wa TPB, Noves Moses alisema hayo jana katika hafla ya kumtangaza mshindi wa simu ya mkononi aina ya Samsung J5, Mohamed Sipe.

Mshindi huyo mkazi wa USA River alishinda katika shindano la kuweka na kutoa pesa kupitia huduma ya Western Union linaloendeshwa na benki hiyo.

Alisema mbali na kutoa huduma mbalimbali za kibenki pia, imekuwa ikitenga fungu maalumu kwa ajili ya kusaidia jamii zenye uhitaji ikiwa ni sehemu ya kurudisha kwa wananchi kile wanachokipata.

Alisema fedha hizo zimetumika kujenga madarasa, zahanati, matundu ya vyoo, kununua madawati, mashuka na vitanda katika hospitali mbalimbali.

“Mwaka ujao tumetenga Sh200 milioni kwa ajili ya kusaidia shughuli za kijamii katika maeneo yetu. Hadi sasa tuna matawi makubwa 30 na madogo 36 nchi nzima,” alisema.

Meneja wa TPB, Tawi la USA River, Speratus Kamala alisema shindano hilo limeanza Oktoba mwaka huu

Mshindi wa shindano hilo, Sipe alisema huwa anatumia huduma ya Western Union mara kwa mara kutuma na kupokea fedha.