TFC, Wachina kuchimba mabwawa ya umwagiliaji

Ofisa mwandamizi uhamasishaji na uwekezaji wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA), Nakadongo Fares akizungumza na wajumbe wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) na wataalamu wa Kampuni ya Juren Group ya China wakati ujumbe huo ulipotembelea kituo hicho juzi. Picha na Salim Shao

Muktasari:

Mbali na kuchimba visima na mabwawa hayo, kampuni hiyo ya Kichina itajenga kiwanda cha uunganishaji matrekta eneo Misugusugu mjini Kibaha ili kuinua sekta hiyo na kuimarisha kipato cha wananchi.

       Dar es Salaam. Katika mkakati wa kuondokana na kilimo cha msimu, Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) kwa kushirikiana na kampuni ya Juren Group ya China wanatarajia kuchimba visima virefu na mabwawa ili kuvuna maji ya mvua kwa ajili ya umwagiliaji.

Mbali na kuchimba visima na mabwawa hayo, kampuni hiyo ya Kichina itajenga kiwanda cha uunganishaji matrekta eneo Misugusugu mjini Kibaha ili kuinua sekta hiyo na kuimarisha kipato cha wananchi.

Mkurugenzi wa ushirika na maendeleo, Henry Mwimbe alisema idadi ya visima na mabwawa yatakayochimbwa itafahamika baadaye lakini dhamira ya TFC ni kuhakikisha maisha ya wanachama wake yanaboreshwa.

“Asilimia 70 ya wananchi ni wakulima wanaotegemea mvua ambayo bado ni changamoto kwa sababu inanyesha msimu mmoja kwa mwaka, hivyo kuvuna ni mara moja.

Inakuwa ngumu kupigana na umaskini na kuzalisha chakula cha kutosha,” alisema Mwimbe.

Alisema uchimbaji wa visima na mabawa hayo utaenda sambamba na utoaji elimu kwa wakulima kuhusu mazao yanayofaa katika maeneo waliyopo.

“Si kila zao unalotaka kulima linaweza kufaa katika eneo ulipo, bali udongo una chembechembe tofauti na aina ya zao ambalo linaweza kustawi,” alisema.

Alisema shirikisho hilo linataka kufuta dhana ya wakulima kulima wanachotaka, badala ya mazao yatakayostawi maeneo waliyopo kulingana na vipimo vya udongo vinavyofanywa na wataalamu.

Ofisa uhusiano mkuu wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA), Nyanda Shuli aliwashauri wawekezaji hao kuwa licha ya uunganishaji matrekta, wajitahidi kuanza uzalishaji wa bidhaa zao nchini.

Kwa upande wao Juren Group, viongozi wake waliahidi kuanza kutengenezea matrekta hayo nchini iwapo mazingira ya uwekezaji yatakuwa mazuri badala ya kuunganisha.