Wanawake walamba dume mikopo Kanda ya Ziwa

Tuesday November 7 2017

Katibu wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji

Katibu wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Beng’I Issa 

By Rehema Matowo, Mwananchi [email protected]

Geita. Makundi ya wanawake yamenufaika kwa kiasi kikubwa na mkopo uliotolewa na taasisi mbili za fedha kwa ushirikiano na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.

Katibu wa baraza hilo, Beng’I Issa alisema kuwa, asilimia 57 ya mkopo huo umeelekezwa kwa makundi yanayoundwa na wanawake, huku yale ya wanaume yakipata asilimia 43.

Miongoni mwa wajasiriamali walionufaika na mikopo hiyo wamo mamalishe, wavuvi, wachimbaji wadogo wa madini, wamachinga na waendesha bodaboda.

Fedha hizo zimetolewa na Benki ya Posta na UTT Microfinance ambazo kwa pamoja zimetoa mkopo wenye riba nafuu wa Sh2.8 bilioni kwa vikundi 277 vya wajasiriamali kutoka Kanda ya Ziwa.

Hundi ya fedha za mkopo huo ilikabidhiwa kwa wawakilishi wa vikundi hivyo na waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Vijana, Jenista Mhagama wakati wa hafla iliyofanya mjini Geita juzi.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mhagama aliwataka wanachama 3,789 wa vikundi vitakavyonufaika na mkopo huo kutumia vyema fedha hizo kuendeleza miradi ya uzalishaji itakayowawezesha kumudu marejesho na hatimaye watu wengi zaidi kukopeshwa.

Waziri huyo aliimwagia sifa Halmashauri ya Mji wa Geita kwa kutoa mikopo ya zaidi ya Sh500 milioni kwa vikundi vya maendeleo vya vijana na wanawake kutokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani na kuziagiza halmashaur nyingine nchini kuiga mfano huo.

“Ni vyema sasa vikundi vya maendeleo vya wananchi kupitia vicoba na saccos vijielekeze kwenye kuanzisha na kuendesha viwanda vidogo na vya kati vinavyotumia malighafi inayopatikana kwenye maeneo yao,” alisema Mhagama.

Pia, aliyaagiza mabaraza ya uwezeshaji kusaidia wananchi kutambua, kufikia na kutumia fursa zilizopo kwenye maeneo yao ili kujikwamua kiuchumi.

Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku aliwataka wanufaika kuitumia vizuri mikopo hiyo.

Advertisement