Kanda Maalum ya Polisi yanukia Pwani

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba

Muktasari:

  • Katika ukurasa wake wa Facebook, Mwigulu alisema kutokana na mauaji ya mara kwa mara  wilaya za Kibiti, Mkuranga na Rufiji Serikali itaangalia upya kuanzisha Kanda Maalumu Polisi.

Kibiti. Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amesema kufuatia mauaji ya Ofisa Upelelezi Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani, Peter Kubezya anayedaiwa kuuawa na majambazi, wanafikiria kuanzisha Kanda Maalumu ya Polisi.

Katika ukurasa wake wa Facebook, Mwigulu alisema kutokana na mauaji ya mara kwa mara  wilaya za Kibiti, Mkuranga na Rufiji Serikali itaangalia upya kuanzisha Kanda Maalumu Polisi.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evaristi Ndikilo aliyewaambia wananchi kuwa Serikali itawatia mbaroni watu wote wanaojihusisha na matukio hayo.

Ndikilo, ambaye kutokana na wadhifa wake anakuwa mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa, alisema wanakwenda kujipanga upya na kuanzisha kanda maalumu itakayokuwa na kikosi kipya kwa ajili ya kupambana na watu wote wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu.

 Ofisa huyo aliuawa pamoja na watu wengine wawili, ambao pia walipigwa risasi katika tukio hilo lililotokea Kijiji cha Jaribu wilayani Kibiti.

Tukio hilo limekuja miezi michache baada ya ofisa mwingine wa polisi, ASP Thomas Njuki, ambaye alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia Ujambazi, kuuawa Vikindu  kwa kupigwa risasi kichwani akiongoza kikosi cha polisi kilichokwenda kujaribu kukamata watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi.