Monday, July 17, 2017

Dk Mpango azungumzia uhusiano wa China na Tanzania

 

By Julius Mnganga, Mwananchi; jmathias@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Licha ya mambo mazuri yaliyofanywa kutokana na uhusiano mwema kati ya China na Tanzania, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema huu ni wakati wa kuutafakari uhusiano huo.

Amesema China imefanya mengi katika kuboresha miundombinu ya usafirishaji, viwanda na kuongeza uwekezaji, huku Tanzania ikikumbukwa jinsi ilivyolisaidia Taifa hilo kuingia Umoja wa Mataifa na hivyo kupata nafasi kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

"Ni uhusiano wa aina gani tunauhitaji kati ya mataifa haya mawili ni kitu muhimu tunachotakiwa kukijadili. Tuangalie fursa za biashara na uwekezaji zilizopo baina yetu na namna zitakavyotunufaisha," amesema Dk Mpango.

Amesema hayo kwenye mkutano wa sita wa mwaka wa Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Uchumi na Jamii (ESRF) ambao mwaka huu umewakutanisha wadau wa biashara na maendeleo kutoka Tanzania na China.

Akielezea fursa za kuimarisha uhusiano huo leo, Julai 17  Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki amesema ipo haja ya kuushusha mpaka mamlaka za chini.

"Ipo wilaya moja China ambayo GDP (pato lake la mwaka) yake ni Dola 50 bilioni za Marekani ambazo ni sawa na GDP ya Tanzania. Kuna fursa kwa halmashauri zetu kuanzisha uhusiano na zile za China," amesema Mbelwa.

-->