Kesi ya aliyekuwa kigogo wa Barclays kusikilizwa mfululizo

Muktasari:

  • Kesi hiyo itaanza kusikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi wao na washtakiwa hao kusomewa maelezo ya awali (PH) jana.

Kasililika anadaiwa kuwasiliana na watuhumiwa wa tukio la ujambazi katika benki hiyo

Dar se Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuanzia Oktoba 3 hadi 5 mwaka huu itaanza kusikiliza kesi ya wizi wa Sh390 milioni, Dola 55,000 za Marekani na Euro 2,150 inayomkabili aliyekuwa meneja wa Benki ya Barclays, Tawi la Kinondoni, Alune Kasililika na wenzake 11.

Kesi hiyo itaanza kusikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi wao na washtakiwa hao kusomewa maelezo ya awali (PH) jana.

Akiwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao, Wakili wa Serikali, Mwanaamina Kombakono alidai kuwa Kasililika aliwasiliana na watuhumiwa wa tukio la ujambazi katika benki hiyo.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Neema Batchu, mfanyabiashara Hamis Shabani au Carlos na dereva Manase Genyeka au Mjeshi.

Wengine ni wafanyabiashara Kakamie Julius, Iddy Khamis, Sezary Massawe, Boniphace Muumba, Ruth Macha na maofisa wawili wa polisi, Iddy na Bundala ambao wanatetewa na wakili Nehemiah Nkoko.

Jana, Kombakono alidai kuwa siku ya tukio Aprili 15, mwaka 2014 asubuhi, mshtakiwa Kasililika na Neema Batchu ambao ni wafanyakazi wa benki hiyo, walifika kazini na shughuli za kibenki ziliendelea pamoja na wafanyakazi wengine.

Alidai kuwa Kasililika siku hiyo ya tukio alikuwa na mawasiliano na mshtakiwa wa tatu hadi wa tisa ili kuandaa tukio la wizi wa fedha za benki hiyo na hatimaye lilifanyika.

Kombakono alidai kuwa wizi ulifanikiwa baada ya washtakiwa hao ambao ni wafanyakazi wa benki hiyo kutoa taarifa za kina kuhusu benki kwa mshtakiwa wa tatu hadi wa tisa.

Alidai kuwa mshtakiwa Ruth Macha anadaiwa kumsaidia mshtakiwa Maulid Seif kutoroka ili kukwepa mkono wa sheria.

Baada ya kumaliza kumsomea maelezo hayo, Hakimu Shaidi alimtaka kila mshtakiwa kujibu anayokubali na anayokataa.

Hata hivyo, washtakiwa wote walikubali maelezo yao binafsi ikiwamo majina na walikana maelezo yote yanayohusu wizi huo.

Katika kesi hiyo, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama na kutenda kosa la wizi wa fedha za Benki ya Barclays.

Inadaiwa kuwa Aprili 15, 2014 kwa unyang’anyi wa kutumia silaha, washtakiwa hao waliiba Sh390 milioni, Dola za Marekani 55,000 na Euro 2,150 mali ya benki hiyo.

Katika shtaka linalowahusu maofisa wa polisi, Iddy na Bundara, wao wanadaiwa kuwasaidia washtakiwa kutoroka ili wasikamatwe na kufikishwa mbele ya mkono wa sheria.