Miili mingine 15 yaopolewa ajali ya Mv Nyerere

Muktasari:

  • Akiwa kwenye eneo la tukio, Mtangazaji wa TBC1 Enock Bwigane amesema ameona miili 15 ikiwa inaopolewa.

Dar es Salaam. Idadi ya watu waliofariki dunia katika ajali ya kivuko cha MV Nyerere kilichozama juzi mchana Septemba 20, 2018 imefikia 151 huku uokoaji ukiendelea.

Akiwa kwenye eneo la tukio, Mtangazaji wa TBC1 Enock Bwigane amesema ameona miili 15 ikiwa inaopolewa.

Jana, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipowasili katika Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe alisema idadi ya waliokufa kwenye ajali hiyo ilikuwa watu 136 hivyo pamoja na iliyoopolewa leo inafanya idadi ya walioopolewa kufikia 151.

Akizungumza akiwa katika eneo la tukio, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amesema miili mingine imeopolewa leo asubuhi Septemba 22, 2018.

“Leo miili mingine imeopolewa lakini bado uopoaji unaendelea,” amesema.

Amesema vikosi vya uokoaji vinaendelea na shughuli ya uokoaji na ikitarajiwa shughuli hiyo kufanyika hadi kesho Jumapili.

“Vikosi vya uokoaji vinafanya kazi yake vizuri na tunaendelea na tunatarajia Mungu akijalia hadi kesho tutakuwa tumekamilish,” alibainisha mkuu huyo wa mkoa.

Mongella amesema kuwa baadhi ya miili imeshatambuliwa huku kazi ya utambuzi akisema inaendelea.

“Hadi jana (Ijumaa Septemba 21, 2018) miili 116 imeshapata ndugu na tunaamini miili mingine itatambulika maana wananchi wanaendelea kuwasili kuja kuitambua,” amesema Mongella.