Mradi wa Aga Khan kupunguza vifo vya mama, mtoto Mwanza

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu (katikati) akikata utepe wakati wa kuzindua mradi wa afya ya uzazi wa mama na mtoto (Impact) unaofadhiliwa na Canada na kutekelezwa na Aga Khan Foundation katika hafla iliyofanyikwa kwenye Uwanja wa Ghandh jijini Mwanza jana. Picha na Jesse Mikofu

Muktasari:

Mradi huo utakaogharimu Sh25.3 bilioni unatekelezwa katika halmashauri za Kwimba, Magu, Misungwi, Nyamagana, Ukerewe, Sengerema, Ilemela na Buchosa, huku ukifadhiliwa na Aga Khan Foundation kwa upande wa Canada na Serikali.

Takwimu za mwaka 2016 zinaonyesha kulikuwa na vifo 556 katika kila vizazi hai 100,000

Mwanza. Serikali imezindua mradi wa kupunguza vifo vya uzazi na watoto wachanga mkoani hapa unaotekelezwa na Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN).

Mradi huo utakaogharimu Sh25.3 bilioni unatekelezwa katika halmashauri za Kwimba, Magu, Misungwi, Nyamagana, Ukerewe, Sengerema, Ilemela na Buchosa, huku ukifadhiliwa na Aga Khan Foundation kwa upande wa Canada na Serikali.

Pia, mradi huo wa miaka minne uliozinduliwa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu utajikita kuimarisha miundombinu na mfumo wa utoaji huduma kwa wajawazito na watoto katika vituo 80 vya huduma mkoani hapa.

Mwakilishi wa AKDN, Edna Selestine alimweleza Waziri Mwalimu kuwa mradi huo utawafikia wanawake 650,000 wenye umri wa kuzaa, watoto wachanga chini ya mwaka mmoja 80,000 na wanaume 300,000.

Pia, utahusisha mafunzo ya kuwajengea uwezo wahudumu wa afya ngazi ya jamii na wanachama wa vikundi vya malezi zaidi ya 700.

“Vyombo vya habari, viongozi wa dini na makundi mbalimbali ya kijamii ni miongoni wadau muhimu watakaoshirikishwa katika utekelezaji wa mradi huu,” alisema Selestine.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Mwalimu aliwataka wadau wengine kujitokeza kushirikiana na Serikali kwa kile alichosema kuwa vifo vya mama na mtoto bado ni changamoto.

Alisema takwimu za mwaka 2016 zinaonyesha kulikuwa na vifo 556 katika kila vizazi hai 100,000 na kusababisha vifo 1,568, kwa mwaka huo.

“Mwaka 2017, vifo vitokanavyo na uzazi vilivyoripotiwa vilikuwa 1,512 wakati jumla ya vifo 612 viliripotiwa kati ya Januari hadi Juni mwaka huu; kimsingi, hali hii haikubaliki,” alisema Mwalimu.

Alitaja baadhi ya sababu za vifo hivyo kuwa ni kinamama kupoteza damu nyingi wakati wa ujauzito, kifafa cha mimba, maambukizi ya bakteria baada ya kujifungua, uchungu kinzani na kukosa huduma bora za afya.

Kwa upande wa watoto, Waziri huyo alitaja sababu kubwa kuwa ni kuharisha, nimonia, homa kali, malaria, utapiamlo na upungufu wa damu.