‘Nje ya ajira walimu hutumia mafao vibaya’

Muktasari:

Ofisa Elimu Taaluma mstaafu Mkoa wa Tanga, Rose Ndangalange ametoa kauli hiyo katika hafla ya kuwaaga walimu 13 waliostaafu iliyoandaliwa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT).

 

Tanga. Walimu kukosa ufahamu wa kuishi nje ya utumishi ni chanzo mojawapo cha wengi kutumia mafao yao vibaya kwa kuanzisha miradi isiyo endelevu wanapostaafu.

Ofisa Elimu Taaluma mstaafu Mkoa wa Tanga, Rose Ndangalange ametoa kauli hiyo katika hafla ya kuwaaga walimu 13 waliostaafu iliyoandaliwa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT).

Amekiomba chama hicho kuweka utaratibu wa kuwajenga kisaikolojia walimu wanapokaribia kustaafu ili watumie vyema taaluma yao na mafao wanayoyapata wawapo nje ya kazi.

Ndangalange ambaye alikuwa miongoni wa wastaafu, amesema kutokana na kukosa ufahamu wa kuishi nje ya utumishi, wengi hutumia mafao yao kuanzisha miradi ambayo baada ya muda mfupi huwamalizia fedha.

“Sisi wastaafu tunaiomba CWT kuweka utaratibu maalumu wa kuwapa elimu ya kuwajengea uwezo walimu wafikishapo miezi mitatu kabla ya kustaafu ambayo itawasaidia kutumia kiinua mgongo chao ipasavyo,” amesema Ndangalange.

“Kuna mambo mawili ambayo huwezi kumshauri mtu afanye, moja ni kupenda au kupendwa lakini kuna kila sababu ya kumjengea uwezo kielimu kujua nini akifanye baada ya kustaafu,” alisema Mwalimu Mustapha.