TRA yafunga maduka Iringa

Baadhi ya maduka yaliyofungwa mjini Iringa kwa madai ya wamiliki wake kutokuwa na mashine za kutolea risiti EFD.Picha na mpiga picha wetu.

Muktasari:

  • Inadaiwa kwamba wafanyabiashara hao wamekaidi agizo hilo la TRA kwa zaidi ya miezi mitatu sasa licha ya kuhamasishwa.

Iringa. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefunga maduka ya wafanyabishara wasiotumia mashine za kielektroniki za EFD.

Hatua hiyo imekuja baada ya maofisa wa TRA kufanya ukaguzi wa kushitukiza katika maeneo mbalimbali ya mji wa Iringa na kubaini uwepo wa wafanyabiashara wanaodaiwa kutokuwa na mashine za kutolea risiti za EFD.

Akizungumza na gazeti hili leo Jumanne, Julai 25 Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Iringa, Lampson Tulianje amesema wafanyabishara hao wamekaidi agizo la Serikali la kutakiwa kuwa na mashine kwa zaidi ya miezi mitatu sasa.

“Tumewapa maagizo, tumewahamasisha kwa zaidi ya miezi mitatu lakini bado wamekaidi agizo letu, uamuzi tuliochukua ni kufunga duka na mara atakaponunua tunamfungulia duka lake,”amesema Tulianje.

Tulinje amefafanuaa kuwa lengo la kufikia hatua hiyo ni kuhimiza wafanyabiashara hao kulipa kodi stahiki kwa kutumia mashine hizo ambazo zina uwezo wa kuweka kumbukumbu vizuri za mauzo ya bidhaa zao.

Pia ametoa wito kwa wafanyabiashara hao kuacha kushindana na Serikali badala yake kuhakikisha wananunua mashine hizo na kuzitumia kwa kuwa hata gharama wanazotumia zinarudishwa na TRA wakati wa kukadiria kodi zao.

“Rai  kwa  wafanyabiashara ni vyema wakanunua mashine zitakazosaidia kuweka vizuri kumbukumbiu za mauzo yao na kuisaidia Serikali kukusanya kodi sahihi, zaidi yote mashine hizo zinatolewa bure na TRA kwa kuwa gharama wanazotumia kununulia mashine zitaunganishwa kwenye makadirio ya kodi yao ya mapato,”amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabishara mkoani hapa, Odilo Ngamiraga amesema wafanyabishara hawajagoma kutumia mashine hizo na kwamba tatizo lipo kwa wasambazaji ambao pindi wanapokwenda huambiwa wasubiri.