‘Takwimu za sukari mwaka jana hazikuwa sahihi’

Muktasari:

Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Adolf Mkenda wakati akifungua mafunzo ya wakusanya takwimu kutoka wilaya mbalimbali nchini.

Dodoma. Takriban mwaka mmoja baada ya sakata la uhaba wa sukari nchini, Serikali imeeleza kuwa takwimu zilizotolewa mwaka jana kuhusu kiwango cha bidhaa hiyo hazikuwa sahihi na badala yake iko kwenye mkakati wa kuhakikisha kasoro hiyo haijirudii.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Adolf Mkenda wakati akifungua mafunzo ya wakusanya takwimu kutoka wilaya mbalimbali nchini.

Profesa Mkenda alisema takwimu zilizopatikana kuhusu sukari zilikusanywa kutoka kwenye viwanda na masoko lakini wakabaini kulikuwa na maeneo ambako kulikuwa na uchochoro wa kupitishia sukari ya magendo.

Alisema hali hiyo ilileta mkanganyiko mkubwa na kusababisha kuwapo kwa takwimu zisizo linganifu kutoka kwa mamlaka mbalimbali.

Mwaka jana, Taifa lilikumbwa na uhaba wa sukari na kusababisha kupanda bei maradufu kutoka wastani wa Sh2,000 hadi Sh4,000 kwa kilo katika baadhi ya mikoa huku Serikali ikiwatuhumu baadhi ya wafanyabiashara kuficha bidhaa hiyo ili iadimike sokoni.