Ubunifu kutumiwa kuchochea maendeleo ya uchumi

Kiongozi wa Mfuko wa maendeleo ya jamii na ubunifu endelevu (HDIF), David B Mc Ginty akizungumza jijini Dar es Salaam jana kuhusu wiki ya ubunifu inayotarajiwa kuanza wiki ijayo. Katikati ni Mkuu wa Idara ya maendeleo ya kimataifa kutoka Serikali ya Uingereza (UK aid), Bethy Arthy na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk Amos Nungu. Picha na Venance Nestory

Muktasari:

  • Kauli hiyo aliitoa jana wakati wa Wiki ya Ubunifu (Innovation Week 2018), iliyoandaliwa na tume hiyo.

Dar es Salaam. Kaimu mtendaji mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk Amos Nungu amesema ubunifu nchini ni chachu ya maendeleo katika sekta zote zinazogusa maendeleo ya jamii na uchumi.

Kauli hiyo aliitoa jana wakati wa Wiki ya Ubunifu (Innovation Week 2018), iliyoandaliwa na tume hiyo.

Tukio hilo hufanyika kwa lengo la kuibua vipaji katika utafiti, maendeleo, ujasiriamali, teknolojia na mitindo.

Pia, husaidia kushawishi na kuwajengea hamasa viongozi wa sasa na wa baadaye kukabiliana na changamoto zinazoibuka kwenye jamii, kushirikiana katika sekta ili kuleta chachu ya mabadiliko kupitia ubunifu.

“Wanataaluma na mashirika mbalimbali ya kisekta watatoa uzoefu katika ubunifu kuhusu sekta mbalimbali, kwa hiyo wiki ya ubunifu katika tume ni muhimu kwa sababu inatoa jukwaa la kuwakutanisha wabunifu nchini na kubadilishana mawazo,” alisema Dk Nungu.

Kiongozi wa Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza (UK Aid) nchini, Beth Arthy alisema wanajivunia kuwezesha wabunifu nchini baada ya kutoa Paundi 40 million ( Sh123 bilioni) kupitia Mfuko wa Ubunifu wa Maendeleo ya Watu (HDIF).

“Tunajivunia kuwezesha ubunifu kuimarisha uchumi wao kupitia HDIF na Costech... kutafuta wadau wapya na kupata hamasa kuhusu umuhimu wa ubunifu,” alisema.

Naye kiongozi mkuu wa HDIF, David McGinty alisema mfuko huo umejikita kuhakikisha unaibua ubunifu utakaokuwa na athari kwa jamii na maisha ya Watanzania.