Uhaba wa pembejeo unavyotishia mavuno ya korosho msimu mpya

Muktasari:

  •  Waziri Tizeba aliifuta CIDTF kutokana na mzozo uliojitokeza kwenye mchakato wa tenda ya kuleta salfa ya unga kwa ajili ya kupulizia kwenye miti ya korosho, ambapo Kampuni ya Bonanza Vietnam iliyoshinda tenda ilikataliwa na mfuko huo kwa kile walichoeleza kuwa wana kesi nayo.

Miezi minane tangu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba kuufuta Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza zao la Korosho (CIDTF) na kuhamishia majukumu yake Bodi ya Korosho (CBT), tayari pengo la pembejeo za zao hilo limejionyesha na kuzua kilio kwa wakulima.

 Waziri Tizeba aliifuta CIDTF kutokana na mzozo uliojitokeza kwenye mchakato wa tenda ya kuleta salfa ya unga kwa ajili ya kupulizia kwenye miti ya korosho, ambapo Kampuni ya Bonanza Vietnam iliyoshinda tenda ilikataliwa na mfuko huo kwa kile walichoeleza kuwa wana kesi nayo.

 Miongoni mwa majukumu ya CIDTF yalikuwa ni kuwatambua wakulima wa korosho na kuwasambazia pembejeo wakulima ambao walitakiwa kuchangia fedha. 

Pamoja na majukumu ya CIDTF kuhamishiwa Bodi ya Korosho, Mei 13 mwaka huu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza katika mkutano wa wadau wa korosho mjini Dodoma alitangaza kutolewa bure kwa pembejeo za zao hilo kwa msimu huu.

Hata hivyo, wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, baadhi ya wakulima walisema kuna hatari ya mavuno kushuka kutokana na upungufu wa salfa ya unga waliyotakiwa kupata.

Ahmed Ulenge ambaye ni mwenyekiti wa chama cha wakulima wa korosho cha Amani Cashewnut, anasema awali CIDTF ilikuwa ikichukua takwimu ya wakulima na mahitaji yao ya pembejeo hivyo ugawaji ulikuwa rahisi.

  “CIDTF walikuwa wanatusaidia kujua takwimu za wakulima na mahitaji yao, lakini Bodi ya Korosho hawafanyi hivyo. Bodi iliundwa kwa ajili ya wakulima, lakini sasa ni chombo cha Serikali, wanakaa tu ofisini,” anaongeza Ulenge.

Naye Somoye Issa ambaye ni mkulima wilayani Tandahimba alikuwa na malalamiko kama hayo akisema bure iliyotangazwa na Serikali sasa inawagharimu. 

“Mimi kwa msimu huu nilihitaji mifuko 12 ya salfa ya unga, lakini nimeletwa mifuko miwili tu. Fedha tulizokuwa tumechanga kwa ajili ya kuletewa salfa zilirudishwa tukaambiwa kuwa tutaletewa bure. Bora hata tungenunua tu.

 “Wakati CIDTF walipokuwepo tulikuwa tunachangia na Serikali nayo inachangia halafu tunaletewa dawa za kutosha, lakini sasa ni matatizo matupu,” anasema Somoye.

 

Kauli ya Ofisa Kilimo

 Ofisa Kilimo na Ushirika wa Wilaya ya Tandahimba, Issa Naumanga anakiri kuwepo kwa upungufu wa pembejeo katika wilaya hiyo, akisema Serikali iliahidi kuondoa tatizo hilo. 

“Mahitaji ya wilaya nzima yalikuwa tani 4,717, lakini wameleta tani 2,880 sawa na asilimia 61. Ila walisema wataongeza na muda wa kupuliza dawa unakwisha,” anasema Naumanga. 

Wilaya ya Tandahimba inaongoza nchini kwa kilimo cha korosho.

 Rashidi Mussa ambaye ni mkulima wa mfano wa korosho anayeishi wilayani Newala anawaunga mkono wakulima wenzake akisema mwaka huu wakulima wengi wataathirika.

 “Ni kweli mahitaji ya safla ya unga ni makubwa mno kuliko Serikali ilivyotarajia. Mbaya zaidi, wale wafanyabiashara waliokuwa wakiuza salfa waliacha baada ya kusikia Serikali itagawa bure,” anasema Mussa.

 “Mimi kwa shamba langu nilihitaji mifuko 300, lakini nimepewa mifuko ya bure 26 tu. Awamu ya kwanza mifuko 14 na ya pili mifuko 12,” anaongeza.

Hata hivyo, anasema kilichomsaidia aliwahi kununua mifuko ya salfa tangu Juni mwaka huu na kuihifadhi kwa ajili ya akiba.

 ‘Baada ya Serikali kutangaza kugawa salfa ya bure ikarudisha fedha za wakulima ambao nao walizitumia kwa mambo mengine wakitumaini kupata salfa ya bure matokeo yake sasa wanalia,” anasema.

Akizungumzia utendaji wa CIDTF, Mussa anasema ulikuwa mzuri na japo walichangia fedha, lakini walipata salfa ya kutosha kwa wakati.

 “CIDTF walitusaidia sana, kwa sababu tulikuwa tunachangia fedha na Serikali nayo inatoa ruzuku, lakini tunapata dawa za kutosha kwa kuwa walikuwa wanafuatilia. Pengine Serikali itajipanga kwa mwakani,” anasema Mussa.

 Akizungumzia malalamiko ya wakulima kukosa pembejeo za kutosha kwa msimu huu, aliyekuwa Mwenyekiti wa CIDTF, Athuman Nkinde anasema kwa utaratibu wa sasa ni vigumu kukidhi mahitaji ya wakulima.

 “Sisi tulikuwa tunawaambia wachangie asilimia 50 ya pembejeo au fedha kidogo kama Sh10, 000 au Sh5,000 ili kuonyesha nia. Kwa sababu hao wakulima hawajawahi kufanyiwa sensa. Sasa ukitangaza kugawa bure, kila mtu anajitokeza hata wasiokuwa wakulima,” anasema Nkinde.

 “Tulikuwa tunafuata ushauri wa wataalamu kwa kununua pembejeo moja kwa moja kiwandani. Tulifanya hivyo kwenye msimu uliopita na tulifanikiwa kukidhi mahitaji. Kwa sasa sijui wamempa tenda nani na anatoa wapi?” anahoji Nkinde.

 Alipoulizwa kuhusu mzozo wao na Bonanza Vietnam, Nkinde anasema kwa sasa hahusiki kwa kuwa CIDTF ilishafutwa. 

“Hiyo kesi waulizwe CBT waliokabidhiwa majukumu yetu, hayo ni mambo ya Serikali sisi tuko nje. Ninavyojua ni kwamba Bonanza Vietnam hawakupewa tenda kutokana na ushahidi wetu,” anasema Nkinde.

 Akijibu lawama hizo, Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho, Hassan Jarufu anasema Serikali ilishatoa tamko wakati wa kilele cha sherehe za Nanenane mkoani Lindi na kumtaka mwandishi kuwasiliana na waandishi wa mkoa huo.

 “Waziri wa Kilimo alishatoa tamko wakati wa Nanenane, muulize mwandishi wenu aliyekuwepo. Serikali ndiyo ilitoa uamuzi wa kugawa pembejeo bure na ikatoa kauli yake pale, waulize wenyewe,” anasema Jarufu.

 Hata alipoulizwa kuhusu mchakato wa tenda, Jarufu aliendelea kusisitiza kuwa aulizwe Waziri Tizeba mwenyewe, huku pia akithibitisha kuwa Kampuni ya Bonanza Vietnam haikupewa.

 “Bonanza haikupewa tenda. Mimi nakujibu tu kwa ufupi, lakini ukimuuliza Waziri mwenyewe atakueleza,” anasema Jarufu.

 Hivi karibuni Chama cha ACT Wazalendo kiliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu kuwapo upungufu wa pembejeo za korosho katika mikoa linapolimwa zao hilo. 

 

Bodi ya Korosho yazungumza

Hata hivyo, akijibu maelezo hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Agosti 3 mwaka huu, Katibu wa Bodi ya Korosho (CBT), Ugumba Kilasa alisema Serikali ilitoa ruzuku ya pembejeo hizo za kutosha kulingana na mahitaji ya wakulima.

“Serikali imetoa ruzuku ya salfa kwa kiwango kilichoagizwa, kwa mkulima anayeona haikidhi mahitaji yake hajakatazwa kununua na ndiyo maana wafanyabiashara bado wanauza,” alisema Ugumba.

Awali katika mvutano huo, Bonanza Vietnam ambayo awali ilijulikana kwa jina la Hammers Inc. Ltd ilidaiwa kushindwa kutimiza masharti ya tenda ya kuleta salfa ya unga yenye thamani ya zaidi ya Sh800 milioni waliyopewa katika msimu wa mwaka 2011/12.

 Katika maelezo yake, Waziri Tizeba aliitetea kampuni hiyo akisema bei yake ni rahisi hivyo itarahisisha upatikanaji wa pembejeo kwa wakulima.

 Akiwa mkoani Lindi wakati wa maadhimisho ya Nanenane, Waziri Tizeba alisema lengo la Serikali kutoa pembejeo bure ni kuwawezesha wakulima kuzipata kwa urahisi.

 Alisema Mkoa wa Lindi uliotakiwa kupata tani 18,000 umepata tani 14,000 tu huku akisema tani 4,000 zilizobaki ziko bandari ya Dar es Salaam, muda wowote zitawafikia wakulima.