‘Ukiwa waziri wizara hizi, hulali vizuri’

Muktasari:

Wizara zingine ni ya Mambo ya Ndani ya Nchi; Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Maliasili na Utalii na Wizara ya Fedha.

Dar es Salaam. Kama ulidhani Profesa Sospeter Muhongo ni waziri pekee aliyewahi kujikuta akiwajibishwa, basi umekosea. Wapo wengine kibao waliopitia wizara zingine nne huku aliyotoka ile ya Nishati na Madini ikiwamo.

Wizara zingine ni ya Mambo ya Ndani ya Nchi; Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Maliasili na Utalii na Wizara ya Fedha.

Wachambuzi wa mambo ya siasa na uchumi wanasema wizara hizo ni nyeti na zinahitaji utendaji wa kiwango cha juu ili kufikia matarajio ya mteuzi, yaani rais kulingana na vipaumbele vya Serikali anayoiongoza.

“Katika mazingira hayo, kunakuwa na mikataba mikubwa, kushinikizwa, tamaa za baadhi ya viongozi. Hivyo kupata ‘watakatifu’ watakaoongoza wizara hizi bila kupata misukosuko itakuwa vigumu,” anasema Dk Benson Bana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Akizungumzia wizara hizo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda anasema wizara hizo zinatakiwa kuwa na mawaziri wabunifu wasiofanya kazi kwa mazoea.

“Hizo ni wizara kubwa zenye masuala muhimu kwa taifa ambayo waziri akikosa ubunifu na asipokuwa makini hawezi hata kumaliza mwaka mmoja kazini,”anasema Mbunda.

“Profesa Muhongo ndiye alitakiwa kuunda kamati kuchunguza mchanga, sasa ukisubiri Rais aunde tume hautabaki salama. Ni lazima uwajibishwe.”

Anasema hata suala la mauaji ya Kibiti na Rufiji, waziri anatakiwa asilale kuepuka kuwajibishwa.

Pia, anasema wakati mwingine mawaziri hao wanatakiwa kuwajibika kwa makosa ambayo yamefanywa na watendaji wa chini.