Upelelezi tuhuma za wizi wa mitihani haujakamilika

Muktasari:

Wakili wa Serikali, Mwanaamina Kombakono leo Oktoba 10, 2018 ameieleza mahakama kuwa upelelezi wa watuhumiwa watano wa wizi wa mitihani ya darasa la saba haujakamilika

Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya kupata mitihani ya taifa ya darasa la saba inayowakabili walimu watano wa shule ya msingi ya kimataifa ya Hazina iliyopo Magomeni katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu bado haujakamilika.

Wakili wa Serikali, Mwanaamina Kombakono aliyaeleza hayo leo Oktoba 10, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Kombakono amedai mahakamani hapo kesi ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado haujakamilika na akaomba ipangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Baada ya kutolewa maelezo hayo, Hakimu Shaidi ameiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 24, 2018.

Washtakiwa hao watano wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo ya Hazina, Patrick Cheche (43), mkazi wa Mapinga Bagamoyo na walimu wake Laurence Ochien (30), Justus James (32), Nasri Mohamed (32) na Mambo Idd (32).

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama ya kuingilia mitihani ya Taifa, kupata na kuwaonyesha watahiniwa maudhui ya mtihani na kufanya mawasiliano na watahimiwa.

Katika shtaka la kwanza washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa Septemba 4, 2018 jijini Dar es Salaam walikula njama kwa kuingilia mitihani ya taifa ya darasa la saba isivyo halali.

Katika shtaka la pili, washtakiwa hao chini ya Sheria ya Baraza la Mitihani la Taifa, wanadai kuwa Septemba 5, mwaka huu, katika shule hiyo ya msingi Hazina, iliyoko Magomeni, Dar es Salaam, kinyume cha sheria walipata uwezo wa kupata mitihani ya Taifa ya darasa la saba na kuonyesha maudhui yake kwa watahiniwa waliosajiliwa wa shule hiyo.

Katika Shtaka la  tatu, washtakiwa hao wanakabiliwa na kosa la kufanya mawasiliano ya maudhui ya mitihani huo kwa watahiniwa ambapo wanadaiwa Septemba 5, mwaka huu, katika shule hiyo, kinyume cha sheria walitoa mitihani kwa watahiniwa waliosajiliwa katika shule hiyo wakati hawakustahili kufanya hivyo.