‘Upinzani wajitathmini hamahama ya wabunge’

Muktasari:

  • Wachambuzi wa masuala ya siasa wamevishauri vyama hivyo kuja na mbinu mbadala ili kuhakikisha vinaendelea kuwapo

Dar es Salaam. Wakati idadi ya wabunge wa upinzani kuhamia CCM imefikia wanne na madiwani zaidi ya 100, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamevitaka vyama hivyo kujitathmini.

Vyama vilivyoathirika na hamahama hiyo ni Chadema, CUF na ACT-Wazalendo. Chadema imekimbiwa na wabunge wanne na CUF wawili huku idadi ya madiwani waliovihama vyama hivyo vitatu ni zaidi ya 100.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wamevishauri vyama hivyo kuja na mbinu mbadala ili kuhakikisha vinaendelea kuwapo kwa kufanya tathmini kwa kasoro walizonazo.

Akizungumza na Gazeti la Mwananchi, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema huenda kuna tatizo linaloendelea ndani ya upinzani na linatakiwa kutafutiwa ufumbuzi haraka.

Dk Bana alitoa mfano wa Chadema akisema licha ya kuwapo udhaifu kutoka nje unaosababisha wanachama wao kuhama, pia kuna tatizo ndani ya chama ambalo hawataki kuliona na kulifanyika kazi.

“Chadema iache kukimbia tatizo wanapaswa kujiuliza kwa nini haya yanatokea wakati huu, inakuwaje makada wao waliokuwa wakionekana waaminifu wanaondoka lazima wajitafakari nini tatizo na wafanye nini kukabiliana nalo,” alisema Dk Bana.

Alifafanua kuwa kama hali itaendelea hivyo, itakuwa ngumu kwao kuwapata watu watakaosimama kupeperusha bendera ya chama hicho mwaka 2020.

“Tunaona sasa hata baadhi ya wabunge ambao ndiyo walikuwa wanapaza sauti nao wamekuwa kimya, lazima kuna kitu kinaendelea,” alisema Dk Bana.

“Wajifungie wafanye tathmini kama hawawezi kujifanyia wawatafute hata watu wa nje wawafanyie tathmini na kuwapa ushauri elekezi, binafsi nipo tayari kufanya hivyo tena bure kabisa kwa sababu hatutaki upinzani ufe,” alisema Dk Bana.

Hoja ya kujifanyia tathmini imeungwa mkono na Dk Richard Mbunda wa UDSM ambaye alisisitiza kuwa hakuna sababu ya wapinzani kuendelea kulalamika bila kutafuta njia ya kurudisha imani yake kwa wananchi.

“Hali ikiendelea hivi na upinzani usipojafanya kitu chochote kurejesha imani kwa wananchi mambo yatakuwa magumu kwao 2020, kuendelea kulalamika sio suluhu wanatakiwa kupambana, siasa ni mapambano,” alisema.

Hata hivyo, Dk Mbunda alisema upinzani bado una muda wa kurekebisha dosari zilizopo na kuja na ubunifu wa vitu ambavyo vitarejesha imani yao kwa Watanzania.

Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu), Gaudence Mpangala alishauri vyama vya upinzani kujiunga na kupingana na hali inayoendelea.

Alisema tatizo lililopo kwa vyama vya upinzani ni kila kimoja kutaka kufanya kazi kivyake, badala ya kujifunza walivyofanya Kenya kuiangusha Kanu.

“Hata Chadema wakija na sera mpya, hawatafanikiwa katika mazingira haya, lazima watatue kiini cha tatizo. Watambue kwamba mkakati uliopo ni kuua upinzani nchini, sasa wakitambua hilo ninaamini watachukua hatua stahiki,” alisema Profesa Mpangala.

Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi alisema: “Kwa kiongozi ambaye amekamilika hawezi kusaliti misimamo yake. Kwani kumuunga mkono Rais ni lazima uhame chama?.”