Tuesday, September 11, 2018

Vijembe vyatawala kampeni za mgombea ubunge wa Chadema

 

By Jackline Masinde, Mwananchi Jmasinde@mwananchi.co.tz

Ukonga. Mkutano wa kumnadi mgombea ubunge Jimbo la Ukonga kwa tiketi ya Chadema uliofanyika juzi viwanaja vya Kivule ulitawaliwa na vijembe vilivyokuwa na lengo la kumkejeli mgombea wa CCM, Mwita Waitara.

Wakizungumza katika kampeni hizo viongozi wa chama hicho wakiongozwa na katibu mkuu Dk Vincent Mashinji walisema Waitara ni msaliti na kwamba ameshindwa hawezi kuwaletea maendeleo.

Mkutano huo ambao uliudhuriwa pia na viongozi wengine wa chama hicho akiwamo mbunge wa Jimbo la Kibamba, John Mnyika, naibu Katibu mkuu Baraza la Wanawake Chadema, Kunti Majala na Mkurugenzi wa Uchaguzi chama cha ACT Wazalendo, Erasto Njuuka walitumia mkutano huo kuwashawishi wananchi kutoichagua CCM kwa madai kuwa haitawaletea maendeleo.

Akizungumza mkurugenzi huyo wa uchaguzi wa ACT Wazalendo, alisema alisema Waitara amewavua nguo wana Ukonga.

Majala akizungumza kwenye mkutano huo wa kampeni, aliwataka wana Ukonga kumkataa Waitara ikiwa ni njia ya kumwajibisha kwa usaliti aliowafanyia.

Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye katika hotuba yake ya kumnadi mgombea wa Chadema, alisema CCM imekosa mvuto kwa wananchi kwani toka imeingia madarakani maisha ya Watanzania yamezidi kuwa magumu.

Sumaye alisema toka CCM iingie madarakani wanawake wanashindwa hata kuuza ndoo moja ya vitumbua, wafanyabiashara wadogo na wakati wanashindwa kukopa fedha benki.

Awali mbunge wa Jimbo la Kibamba, John Mnyika aliwataka wananchi kumpa kura mgombea wa chama hicho, Asia Msangi ili aweze kuongeza nguvu bungeni.

“Nasikia mmenyang’anywa kiwanja cha shule, mpeni kura zote Msangi akajenge hoja bungeni ili mrudishiwe kiwanja chenu, kuna ujenzi wa daraja la Kivule mkimchagua Waitara daraja hili halitajengwa maana jimbo hili limetawaliwa na CCM miaka mingi halikujengwa,” alisisitiza.

Msangi akiomba kura kwa wananchi alisema hana Sh5,000 za kumpa kila mtu, hana kanga wala kahawa ila anaomba kura ili awalipe maendeleo.

-->