Viongozi upinzani waunga mkono hoja ya Lowassa

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Muktasari:

  • Juzi Lowassa alikaririwa na Mwananchi akisema kuendelea na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iliyopo sasa ni sawa na kufanya CCM iwe inatangazwa mshindi katika kila uchaguzi kauli ambayo ilijibiwa jana na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Kaijage akisema “Hayo aliyoyasema (Lowassa) ni maoni yake.”

Dar es Salaam. Viongozi wa vyama vya upinzani wameunga mkono hoja iliyotolewa na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kwamba umefika wakati wa kuwa na tume huru ya uchaguzi nchini.

Juzi Lowassa alikaririwa na Mwananchi akisema kuendelea na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iliyopo sasa ni sawa na kufanya CCM iwe inatangazwa mshindi katika kila uchaguzi kauli ambayo ilijibiwa jana na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Kaijage akisema “Hayo aliyoyasema (Lowassa) ni maoni yake.”

Lowassa alisema mambo manne yanatakiwa kufanyika ili kuwa na uchaguzi huru kubwa likiwa kuwa na tume huru ya uchaguzi.

Akizungumza jana katika mkutano uliowakutanisha viongozi wa vyama vya siasa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa jijini hapa, Profesa Ibrahim Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Msajili, alisema hali ya uchaguzi nchini ni mbaya na chama chake kitaandaa siku maalumu kusudi kitoe tamko.

Aliungwa mkono na Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Yeremia Maganja aliyesema NEC haishirikishi watu katika uendeshaji wake na inaundwa na Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM.

Alisema Tume hiyo imekuwa haichukui hatua dhidi ya malalamiko yanayotolewa na vyama vya upinzani.

“Rais mwenyewe alisema atahakikisha ifikapo 2020 upinzani unatoweka nchini. Kwa hiyo hatushangai haya yanayotokea sasa,” alisema.

Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi alisema muundo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi wa kutumia wakurugenzi kusimamia uchaguzi unaifanya isiwe huru kwa sababu wanawajibika kwa mamlaka ya uteuzi.

Muabhi alipendekeza iondoke kwenye mikono ya Serikali na iundwe tume huru itakayowaondoa wakurugenzi kama wasimamizi wa uchaguzi na ihusishe wadau wengine.

Naibu Katibu Mkuu wa ADC, Queen Sendiga alisema mazingira ya ushindani kwa sasa siyo sawa na watu ambao wana wajibu wa kusimamia uchaguzi ni makada wa CCM.

“Tume ya uchaguzi siyo huru kwa sababu wasimamizi wake ni wakurugenzi, waajiriwa wa Serikali... Sasa hapo tuna Tume ya Uchaguzi kweli?” alihoji.

Katibu Mkuu wa chama cha Sauti ya Umma (Sau), Kisena Kisena alisema kila siku wamekuwa wakiilalamikia Tume kwa kuwa inawakilisha matakwa ya Rais ambaye amepewa mamlaka makubwa ya kuunda chombo hicho wakati yeye pia ni kiongozi wa chama cha siasa.

Majibu ya NEC kwa Lowassa

Akizungumza na Mwananchi jana, Jaji Kaijage alisema “Hayo aliyoyasema (Lowassa) ni maoni yake.”

Alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi anayoiongoza inaendesha uchaguzi kwa kuzingatia Katiba na sheria, “Ifahamike alichokisema (Lowassa) hata hukutakiwa kuniuliza mimi, ungewauliza Rais au Bunge.”

“Tume ipo kwa mujibu wa Katiba na maofisa wake wapo kwa mujibu wa sheria na hakuna kilicho nje ya Katiba au sheria na hiki ndicho kilichopo na hakuna kilichovunjwa mpaka sasa.”

Jaji Kaijage alisema kama kuna tatizo katika michakato ya uchaguzi, kupatikana kwa washindi, sheria ziko wazi wahusika wanaweza kuchukuliwa hatua kwa kufika katika vyombo vya sheria na si kukimbilia kwa waandishi wa habari.

“Kama madai wanayoyatoa yana ukweli, wanaweza kwenda kuyathibitisha mahakamani na kama yana ukweli, uchaguzi unaweza kutenguliwa na sio wabaki kuzungumza na ‘media’ tu, sasa wanapaswa kuchukua hatua ili kuyathibitisha hayo wanayoyasema,” alisema.

Akisisitiza, Jaji Kaijage alisema, “Tume haifanyi mambo kwa matakwa yake, inatekeleza kila kitu kwa mujibu wa Katiba, sheria, kanuni na miongozo yetu na Tume haijawekwa juu ya sheria.”

Jaji Kaijage alikuwa akijibu hoja zilizotolewa juzi na Lowassa aliyetoa maoni ya kuhusu kile kilichojitokeza kwenye uchaguzi mdogo wa Monduli, Ukonga na kata 23, akisema suluhisho la kuwa na uchaguzi huru ni kuwa na tume huru ya uchaguzi, vinginevyo CCM itaendelea kutangazwa kuwa imeshinda katika kila uchaguzi.

“Kama hatuwezi kuwa na tume huru ya uchaguzi, CCM itakuwa inatangazwa imeshinda kila siku, kwa sababu sheria inasema anayetangazwa na tume ndiyo anakuwa ameshinda,” alisema.

Alisema ili kufanya uchaguzi huo uwe wa huru na haki, lazima kuwe na sheria ambayo itafanya tume iwe inabanwa. “Lazima kuwe na chombo ambacho kinaibana tume, lakini sasa tume haiwezi kubanwa.”

Lowassa ambaye alijiunga na Chadema Julai 28, 2015 siku chache kabla ya Uchaguzi Mkuu alisema, “Maofisa na wakurugenzi wanaosimamia uchaguzi, wanateuliwa na Rais na wana wajibu wa kumtii Rais,” alisema Lowassa, ambaye alikuwa waziri mkuu wa kwanza wa Awamu ya Nne.

“Wakurugenzi wengi walioteuliwa ni makada wa CCM ambao walianguka katika uchaguzi wa ubunge mwaka 2015, Rais akawateua, usitarajie kama wapo huru hao,” alisema.

Katika uchaguzi wa Jumapili iliyopita, CCM iliibuka mshindi kwenye majimbo ya Ukonga ambako Mwita Waitara alishinda na Jimbo la Monduli alikoweka kambi Lowassa wakati wote wa kampeni, Julius Kalanga alitetea nafasi yake huku kata zote 23 zikienda CCM