‘Vyama vya ushirika vinafaa kuchochea ukuaji uchumi’

Makamu Mkuu wa Chuo cha Ushirika Moshi (MoCU), Profesa Faustine Bee

Muktasari:

  • Bee ameyasema hayo leo Jumanne, Agosti 15 wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye warsha fupi yenye lengo la kujenga mtazamo chanya juu ya ushirika.
  • Amesema kuwa suala la ushirika ni dhana sahihi na ni mfumo mzuri wa kukuza uchumi kupitia vyama vya ushirika.

Moshi. Wakati Serikali ikiendelea na mchakato wa kuelekea Tanzania ya viwanda, Makamu Mkuu wa Chuo cha Ushirika Moshi (MoCU), Profesa Faustine Bee amesema kuwa vyama vya ushirika vina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi.

Bee ameyasema hayo leo Jumanne, Agosti 15 wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye warsha fupi yenye lengo la kujenga mtazamo chanya juu ya ushirika.

Amesema kuwa suala la ushirika ni dhana sahihi na ni mfumo mzuri wa kukuza uchumi kupitia vyama vya ushirika.

Amesema kwa sasa ushirika huonekana kama ni kitu kibaya kutokana na ubadhirifu unaofanywa na watu wachache wenye nia mbaya na vyama hivyo.

Bee amesema kuwa kupitia waandishi wa habari Watanzania wanatakiwa kujenga mtazamo chanya katika kufikia malengo ya maendeleo ya ushirika hapa nchini.

Amefafanua kuwa ushirika ndiyo njia pekee yenye usawa ya kujenga uchumi utakaomilikiwa na Watanzania.

"Ushirika utaweza kujenga uchumi utakaomuondoa Mtanzania katika umaskini na kumuwezesha kumiliki rasilimali za nchi," amesema Bee.

Naye, Naibu makamu Mkuu wa chuo hicho, Goodluck Mmari amesema duniani kote hakuna njia iliyoonekana kumkomboa maskini zaidi ya ushirika.

Hata hivyo, amesema kuwa kuna matukio yanayotokea katika vyama vya ushirika ambayo yanahusishwa na chuo hicho jambo ambalo siyo sahihi.