#WC2018: Mechi ya kwanza tu, wakang’ara

Muktasari:

Hakuna aliyedhani wala kutarajia kama Russia ingeweza kupata ushindi wa kishindo katika mechi ya ufunguzi

Wakati mechi za raundi ya pili ya Fainali za Kombe la Dunia zikiendelea kupigwa, wapo wachezaji ambao wameng’ara hadi sasa, baada ya mchezo mmoja na wengine katika michezo yote miwili, kwa nafasi mbalimbali.

KUNDI B

Ureno 3-3 Hispania

Huu ulikuwa mchezo wa kwanza wa Kundi B, kabla ya kuchezwa kwa mchezo huu tayari ulivuta hisia za mashabiki wa soka ulimwenguni. Katika mchezo huo, Critiano Ronaldo, ndiye aliyeng’aa zaidi alikitumikia vyema cheo cha unahodha wa timu aliifungia Ureno mabao mawili ya kusawazisha kabla ya kufunga bao lililoiweka mbele na kuwafanya washambuliaji wa Hispania kupambana kusaka bao la kusawazisha kuufanya mchezo huo kumalizika kwa sare ya mabao 3-3 na Ronaldo akiwa wamefunga ‘hat-trick’.

KUNDI A.

Russia 5-0 Saudi Arabia.

Hakuna aliyedhani wala kutarajia kama Russia ingeweza kupata ushindi wa kishindo katika mechi ya ufunguzi hasa ikizingatiwa kuwa historia inaonyesha mara nyingi timu wenyeji huanza vibaya mechi za ufunguzi wa Kombe la Dunia.

Hata hivyo, ilikuwa ni tofauti kwa Russia, wenyeji hawa walitoa kisago cha aina yake kwa Saudi Arabia wakiipiga mabao 5-0 kabla ya kuilaza Misri 3-0. Wachezaji wa Russia walifanya makubwa lakini aliyeng’ara zaidi katika mchezo huo wa kwanza alikua ni kiungo wa CSKA Moscow ya Ligi Kuu nchini Russia, Aleksandr Golovin.

Katika mchezo huo, Golovin sio tu kwamba alifunga bao la kuongoza lakini alifanya makubwa kuchagiza ushindi huo akipika mabao mengine mawili.

Kundi C

Peru 0 - 1 Denmark

Mchezo wa kwanza Kundi C baina ya Peru na Denmark, uliomalizika kwa Peru kupoteza mchezo huo kwa mabao 2-1 kikwazo kikubwa kwa timu hiyio kutoka Amerika ya Kusini alikua ni kipa wa Denmark, Kasper Schmeichel.

Kipa huyu alifanya kazi kubwa akipangua mashuti yote yaliyoelekezwa langoni mwake kiasi cha kuwafanya wachezaji wenzake kumbeba Schmeichel wakimuona kuwa shujaa wao baada ya kumalizika kwa mchezo huo.

Sio tu wachezaji walimbeba lakini hata wachambuzi wa soka na mashabiki walikiri kuwa Schmeichel, ndiye aliyeiwezesha nchi yake kuibuka na ushindi katika mchezo huo.

Kundi D

Argentina 1 - 1 Iceland

Achana na suala la Luka Modric kupika mabao yote waliyopata vinara wa Kundi D, Croatia, katika mchezo wa ufunguzi wala usizungumzie suala la walinzi wa Iceland kumdhibiti Lionel Messi asiichezeshe timu na kupata matokeo, aliyebadilisha mtazamo na kulifanya Kundi D kuonekana kuwa ndilo kundi la kifo ni kipa Iceland, Hannes Thor Halldorsson.

Alimfanya mshambuliaji wa Argentina, Sergio Kun Aguero, kujipigiza chini kwa hasira baada ya shuti lake kali alilofumua akiwa kama mita sita kutoka langoni, kupanguliwa na Halldorsson.

Kundi E

Costa Rica 0-1 Serbia

Hakuna aliyejali wala kuzungumzia mchezo huu wa Kundi E kwa kuwa kabla ya kupigwa wachambuzi wa soka na vituo vya televisheni vilikuwa vikitoa nafasi kubwa za kuwajadili zaidi Brazil ambao pia wapo kundi hili.

Hata hivyo, matokeo ya kushangaza ya sare ya bao 1-1 kati ya Brazil na Uswisi yakawasukuma baadhi yao kuuchambua ushindi wa Serbia na ndipo walipobaini ushujaa wa mshambuliaji chipukizi wa Serbia, Sergej Milinkovic-Savic.

Kundi F

Ujerumani 0-1 Mexico

Kipigo cha kustusha na ambacho kitaingia kwenye rekodi walichokipata mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia, Ujerumani kutoka kwa Mexico, kuliwafanya wengi kuachwa midomo wazi.

Hata hivyo siri ya ushindi wa Mexico inatokana na kasi na chenga za maudhi za winga chipukizi wa Mexico, Hirving Lozano mwenye miaka 22 ambaye aliwapa wakati mgumu walinzi wazoefu wa Ujerumani akina Jerome Boateng, ambao umahiri wao uliipa nchi hiyo ubingwa wa dunia miaka minne iliyopita.

Televisheni kadhaa ziliomba kufanya mahojiano maalumu na Hirving Lozano lakini msimamo mkali wa wakuu wa msafara wa Mexico katika fainali hizo ukawagomea kwa hoja kuwa haifai kufanya mahojiano kwa sasa na kinda huyo anayekipiga kwenye klabu ya PSV Eindhoven ya Uholanzi, kutamuondoa mchezoni.