‘Wanaoibiwa, kutukanwa mtandaoni waende polisi’

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa

Muktasari:

NUKUU

“Ukiibiwa au kutukanwa kupitia simu yako nenda polisi ili upate haki yako na siyo kwenda sehemu nyingine.”

Kamanda Mwakalukwa

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kutoa taarifa kwenye vituo vya polisi wanapofanyiwa uhalifu wa mtandao, badala ya taarifa hizo kuzipeleka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa alisema makosa ya jinai yaripotiwe polisi na si TCRA.

Mwakalukwa alisema wananchi wanapotukanwa na kuibiwa kwa njia ya mtandao wamekuwa wakiripoti TCRA na kwenye vyombo vya habari kinyume na utaratibu. Alisema lengo la polisi ni kupambana na makosa ya mtandao ili kuyapunguza na kwamba watafanikiwa ikiwa watapata ushirikiano kutoka katika jamii.

“Ukiibiwa au kutukanwa kupitia simu yako nenda polisi ili upate haki yako na siyo kwenda sehemu nyingine,” alisema.

Mwakalukwa alifafanua kuwa ukitoa taarifa polisi wao ndiyo watashirikiana na mamlaka hiyo katika masuala ya upelelezi ili kuwabaini wahalifu.

Alisema kwa sasa makosa ya uhalifu wa mtandao yanapungua ikilinganishwa na mwaka uliopita kutokana na jamii kuelimishwa.

Hata hivyo, Mwakalukwa alisema pamoja na matukio hayo kupungua bado wananchi wanatakiwa kuwa makini katika matumizi ya simu za mkononi.

Akitoa takwimu alisema mwaka 2016 kulikuwa na matukio 911 ya kutukana matusi kupitia simu za mkononi, lakini katika kipindi cha Januari hadi Juni 2017 kumekuwa na matukio 327.

Alisema mwaka 2016 matukio ya wizi kupitia mtandao wa simu za mkononi yalikuwa 3,233 lakini katika kipindi cha miezi sita Januari hadi Juni mwaka huu kumekuwa na matukio 1,663.

Alisema mwaka 2016 kulikuwa na matukio 260 ya wizi kwenye mashine za kutolea fedha (ATM), lakini katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu idadi ya makosa hayo ni chini ya nusu ya makosa yaliyotokea mwaka jana. Mwakalukwa alisema pamoja na kwamba matukio yamepungua, wanaendelea kushirikiana na TCRA ili kuwaelimisha wananchi.

Connie Francis ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Tehama wa TCRA alisema mabadiliko ya teknolojia yamesababisha wahalifu nao kuiba kwa njia ya mtandao.

Alisema jambo la msingi ni wananchi kuchukua hatua mapema kwa kutoa taarifa polisi na kutumia simu huku wakifuata Sheria za Makosa ya Mtandao.

“Makosa ni yaleyale lakini kilichobadilika na teknolojia, siku hizi ukitukanwa kwa njia ya mtandao dunia nzima inajua kwamba umetukanwa,” alisema.