Watu wasiojulikana watajwa ripoti ya LHRC

Muktasari:

Ripoti hiyo iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) imemtaja Mwandishi wa Mwananchi, Azory Gwanda aliyetoweka tangu Novemba 21 mwaka jana kuwa ni miongoni mwa waathirika wa watu wasiojulikana na hivyo kusababisha, taharuki miongoni mwa wanahabari.

Ripoti yaeleza kuwa haki ya kuishi ilivunjwa zaidi mwaka jana ikilinganishwa na mwaka 2016

Dar es Salaam. Suala la watu wasiojulikana kutajwa katika matukio ya mauaji na utekaji wa binadamu limeibuliwa kwa mara ya kwanza nchini katika Ripoti ya Haki za Binadamu ya mwaka 2017.

Ripoti hiyo iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) imemtaja Mwandishi wa Mwananchi, Azory Gwanda aliyetoweka tangu Novemba 21 mwaka jana kuwa ni miongoni mwa waathirika wa watu wasiojulikana na hivyo kusababisha, taharuki miongoni mwa wanahabari.

Mambo mengine yaliyotajwa kwenye ripoti hiyo ni mauaji ya kujichukulia sheria mkononi yaliyopoteza watu 917 mwaka jana, mauaji ya vikongwe, ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto ikiwamo ubakaji na ulawiti.

Akisoma ripoti hiyo jana jijini Dar es Salaam, mmoja wa watafiti wa haki za binadamu, Fundikira Wazambi alisema haki ya kuishi ilivunjwa zaidi mwaka jana ikilinganishwa na mwaka 2016 huku ‘mzimu’ wa watu wasiojulikana ukiibuka.

Alisema sababu ya uvunjaji wa haki hiyo ni mauaji ya kujichukulia sheria mkononi, mauaji yanayofanywa na vyombo vya dola sambamba na yale yatokanayo na imani za kishirikina.

Fundikira alisema kwamba Dar es Salaam ndiyo inayoongoza kwa kuwa na matukio mengi ya kujichukulia sheria mkononi ikifuatiwa na Mbeya, Mara, Geita, Tanga na Kigoma.

“Kukosekana kwa imani ya vyombo vya usimamizi wa haki ikiwamo polisi na Mahakama kwa sababu ya rushwa imechangia watu kujichukulia sheria mkononi,” alisema Fundikira.

Alifafanua kuwa kulikuwa na matukio ya kutisha kule Kibiti mkoani Pwani ambako pia askari polisi 12 walishambuliwa na kuuawa kikatili,” alisema.

Akiichambua ripoti hiyo, mwanaharakati wa haki za binadamu, Imelda Urio alisema kumekuwa na uvunjifu wa haki ya kuishi unaotokana na watu wasiojulikana.

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Fatma Karume alisema: “Kwa wastani wakili mmoja anahudumia takribani watu 25,000, ninapata hofu kwa Watanzania kuendelea kukosa uwakilishi wa kisheria.”

Alisema Serikali haiwezi kukwepa jukumu la kutenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanapata haki hiyo mahakamani ili kutatua hiyo changamoto.

Pia, alisema TLS si mali ya umma na imekuwa ikiendelea kusaidia katika kuhakikisha wananchi wanapata haki hiyo.