Wawakilishi wapitisha bajeti Ofisi ya Rais

Mwakilishi wa jimbo la Konde Mkoa wa Kaskazini Pemba,  Omar Seif Abeid akichangia hutuba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba Sheria, utumishi wa umma na utawala bora katika mwaka wa fedha 2018/19 kwenye ukumbi wa Baraza la wawakilishi Chukwani nje kidogo ya mji wa Unguja. Picha na Muhammed Khamis.

Muktasari:

Waziri wa wizara hiyo, Haroun Ali Suleiman aliwasilisha bajeti hiyo juzi akisema kati ya fedha hizo, Sh15 bilioni zitatumika kwa ajili ya mishahara, Sh11.4 bilioni zitakuwa za matumizi mengine ya wizara na Sh1 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Zanzibar. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi visiwani hapa wamepitisha bajeti ya Sh27.5 bilioni ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Katiba Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mwaka 2018/19.

Waziri wa wizara hiyo, Haroun Ali Suleiman aliwasilisha bajeti hiyo juzi akisema kati ya fedha hizo, Sh15 bilioni zitatumika kwa ajili ya mishahara, Sh11.4 bilioni zitakuwa za matumizi mengine ya wizara na Sh1 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Vipaumbele katika matumizi hayo ni uchunguzi wa vitendo vya rushwa, kukuza na kuendeleza ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka na kukiendeleza kituo cha mafunzo ya huduma za kisheria .

Pia, alisema wamekusudia kuimarisha zaidi kitengo cha kuzuia na kupambana na rushwa kwa lengo la kuona wananchi wote wanaishi kwa usawa.

Akitoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja za wajumbe, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Said Hassan Said amepokea changamoto zote na kuahidi kuzifanyia kazi.