Hatima ya dhamana ya Lwakatare kujulikana Kisutu leo

Wilfred Lwakatare

Muktasari:

Lwakatare na Ludovick wanakabiliwa na mashtaka manne yakiwamo ya kula njama ya kutoa sumu kwa nia ya kumdhuru, Dennis Msacky, kushiriki kupanga njama za utekaji nyara, kushiriki katika mkutano wa kupanga kitendo cha ugaidi cha utekaji nyara na kuhamasisha

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, leo itatoa uamuzi kuhusu suala la dhamana kutokana na hoja zilizowasilishwa na mawakili wa upande wa mashtaka na utetezi kuhusu Mkuu wa Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare na mwenzake Ludovick Rwezaura.

Lwakatare na Ludovick wanakabiliwa na mashtaka manne yakiwamo ya kula njama ya kutoa sumu kwa nia ya kumdhuru, Dennis Msacky, kushiriki kupanga njama za utekaji nyara, kushiriki katika mkutano wa kupanga kitendo cha ugaidi cha utekaji nyara na kuhamasisha.

Hakimu Mkazi, Emilius Mchauru anatarajia kutoa uamuzi huo baada ya mawakili watano wanaomtetea Lwakatare akiwamo wakili Peter Kibatala, Mabere Marando, Prof Abdallah Safari, Nyaronyo Kicheere na Tundu Lissu kuomba mahakama kumpa dhamana mteja wao.

Akiwasilisha hoja, wakili wa utetezi Kibatala aliiomba Mahakama kutoa dhamana kwa mteja wao kulingana na mazingira husika na kwamba izingatie kuwa dhamana ni haki ya msingi ya washtakiwa.

Kibatala alidai kuwa ugaidi siyo kosa dogo ni kitu kikubwa iwapo chombo cha kisheria kinachukua haki ya mtu ya dhamana ni lazima kuwapo na sababu zinazojitosheleza kuwa mtu huyu kweli ni hatari na mahakama iridhie kweli ni hatari anyimwe dhamana.

Wakili Lissu aliunga mkono hoja za wakili Kibatala. Kwa upande wa Wakili Safari aliiomba mahakama ichukue kumbukumbu kuwa vitendo vya kubambikia kesi watu vimekithiri katika nchi hii.

Hoja hizo ziliwasilishwa mahakamani hapo na mawakili wa utetezi baada ya Wakili wa Serikali Mkuu, Prudence Rweyongeza kuieleza mahakama kutotoa dhamana kwa washtakiwa hao kwa sababu kesi ya kigaidi haina dhamana na kwamba mahakama hiyo haina uwezo wa kuisikiliza kesi hiyo.

Washtakiwa hao walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo juzi wakikabiliwa na mashtaka manne likiwamo la kula njama ya kutenda kosa la jinai la kutoa sumu kwa nia ya kumdhuru Msacky ambaye ni Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi.

Akisoma hati ya mashtaka, Wakili Rweyongeza alidai kuwa washtakiwa hao walifanya kosa la kula njama na kutenda makosa ya jinai kinyume na kifungu cha 384 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho 2002.

Rweyongeza alidai kuwa Desemba 28, mwaka jana katika eneo la King’ong’o, Wilaya ya Kinondoni, washtakiwa hao kwa pamoja walikula njama kwa kutoa sumu kwa nia ya kumdhuru Msacky ambaye ni Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi kinyume na kifungu cha 227 cha sheria ya kanuni ya adhabu.

Wakili huyo wa Serikali katika shtaka la pili alidai kuwa washtakiwa hao kwa pamoja walikula njama ya kufanya kosa la jinai kinyume na kifungu cha sheria cha 24 (2) cha sheria dhidi ya ugaidi sura ya 21 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002. Alidai kuwa washtakiwa hao,

Desemba 28,2012 walishirikiana kupanga njama za utekaji nyara dhidi ya Msacky kinyume na kifungu cha 21 cha sheria inayopinga ugaidi.

Katika shtaka la tatu, washtakiwa hao wanadaiwa kufanya mkutano wa vitendo vya kigaidi kinyume na kifungu cha 5 (a) cha sheria namba 21 inayopinga ugaidi iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.Aliendelea kudai kuwa siku hiyo ya tukio, washtakiwa hao walipanga na kushiriki katika mkutano wa kupanga kitendo cha ugaidi cha utekaji nyara dhidi ya Msacky.
Kwa mujibu wa shtaka la nne, Lwakatare anadaiwa kuhamasisha vitendo vya ugaidi.