Stone 5 Modern Taarabu yazaliwa

Mashabiki na wapenzi wa muziki wa taarabu wakijinafasi

Muktasari:

Kundi hilo lilidhihirisha ubora wake lilipowatia kiwewe mashabiki waliojitokeza wakati likizinduliwa kwenye uwanja wa nyumbani kwa Mwanahela, Mtaa wa Majengo jijini Tanga.

Tanga. Gwiji wa muziki wa taarabu Afrika Mashariki, Mwanahela Salim ameibuka upya na kudhihirisha kwamba yeye bado lulu baada kuanzisha kundi jipya la Stone 5 Modern Taarabu.

Kundi hilo lilidhihirisha ubora wake lilipowatia kiwewe mashabiki waliojitokeza wakati likizinduliwa kwenye uwanja wa nyumbani kwa Mwanahela, Mtaa wa Majengo jijini Tanga.

Mwanahela ambaye miaka ya 1980 alijipatia umaarufu kwa nyimbo zake ukiwamo, ‘Chonge Mame Nane’, juzi usiku wakati wa uzinduzi wa Stone 5 Modern alidhihirisha umahiri wake kwa kuanza na wimbo wa wakati huo uitwao, ‘Nimezama Kimapenzi’.

Pamoja na Mwanahela waimbaji wengine wanaounda kundi hilo ni Hamza Mussa, Zainabu Mdungi, Mishi Omar, Aisha Ramadhani na Athumani Kidege wakati wapapasa kinanda ni Akida Mohamed na Juma Said, huku gitaa la besi likipigwa na Shaaban Unyeke.