Kamati ya Mufti yashtukia ulaji mali za Bakwata, ‘yapiga pini’

Muktasari:

Agosti 9, mwaka huu, Sheikh Zubeir aliunda kamati ya wajumbe nane kwa ajili ya kushughulikia masuala mbalimbali, ikiwamo misamaha ya kodi iliyoombwa na Bakwata na taasisi zake.

Dar es Salaam. Kamati ya Bakwata iliyoundwa na Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir kufuatilia mali za baraza hilo imepiga marufuku kuuzwa na kupangisha hadi itakapomaliza uchunguzi wake.

Agosti 9, mwaka huu, Sheikh Zubeir aliunda kamati ya wajumbe nane kwa ajili ya kushughulikia masuala mbalimbali, ikiwamo misamaha ya kodi iliyoombwa na Bakwata na taasisi zake.

Kamati hiyo inaongozwa na Sheikh Abuubakar Khalid akiwa mwenyekiti, Sheikh Issa Athman Issa (Makamu) na Mwalimu Ahmed Abeid (Katibu).

Waraka uliotolewa jana na kamati hiyo kwenda kwa masheikh wa mikoa na wilaya ulieleza kwamba kiongozi yeyote wa Bakwata haruhusiwi kuingia mkataba wa kuuza na kupangisha nyumba za baraza hilo.

Pia, kamati ilipiga marufuku kuhamisha mali yeyote au kuingia ubia na mwekezaji au kuingia mikataba mipya, hadi pale kamati hiyo itakapomaliza kazi yake.

Waraka huo ulisisitiza kuwa agizo hilo ni halali kwa mujibu wa Katiba ya Bakwata na linapaswa kufanyiwa kazi ipasavyo.