Watoto wanne wasaidiwa baiskeli baada ya gazeti la Mwananchi kutoa taarifa zao

Muktasari:

Watoto hao ambao hawaongei wala kutembea isipokuwa kutambaa, wanatoka katika kijiji cha Kibululu, Kata ya Kiparang’anda wilaya ya Mkuranga.

Dar es Salaam. Baada ya kukaa kwa muda mrefu bila kupata msaada, hatimaye leo watoto wanne wa familia moja waliozaliwa na ulemavu wa kudumu wamepatiwa baskeli za magurudumu mawili ili ziweze kuwasaidia.

Watoto hao ambao hawaongei wala kutembea isipokuwa kutambaa, wanatoka katika kijiji cha Kibululu, Kata ya Kiparang’anda wilaya ya Mkuranga.

Akikabidhi msaada huo wa baiskeli nne, Mkuu wa  Wilaya ya Mkuranga, Philberto Sanga alisema taarifa za watoto hao walizipata kupitia Gazeti la Mwananchi.

Sanga alisema baskeli hizo zimetolewa na Naibu waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, kazi, Vijana ,Ajira na Walemavu, Dk Abdallah Possi baada ya gazeti hilo kuandika makala kuhusiana na ulemavu wa watoto hao.

Baba mzazi wa watoto hao, Hamisi Sabili(50) alisema huo ni msaada wake wa kwanza tangu azae watoto hao miaka 17 iliyopita na kwamba bado anahitaji msaada zaidi kutokana na watoto wake kuwa na mahitaji mengi.

Agosti 21, mwaka huu gazeti la Mwananchi lilichapisha makala iliyoelezea watoto hao yenye kichwa cha habari 'Nimezaa watoto saba, wanne walemavu wa kudumu'