Viwanda vidogo vyatoa matumaini mapya Mara

Muktasari:

Licha ya baadhi ya viwanda vya kati na vikubwa kufungwa mkoani Mara, uwepo wa viwanda vingi vidogo huenda ukaleta matumaini mapya ya kukuza ajira na uchumi wa mkoa huo iwapo Serikali itaongeza kasi kuboresha mazingira ya biashara.

Musoma/Dar es Salaam. Licha ya baadhi ya viwanda vya kati na vikubwa kufungwa mkoani Mara, uwepo wa viwanda vingi vidogo huenda ukaleta matumaini mapya ya kukuza ajira na uchumi wa mkoa huo iwapo Serikali itaongeza kasi kuboresha mazingira ya biashara.
Matumaini hayo yanakuja baada ya takwimu za Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) kuonyesha kuwa uwekezaji wa viwanda vidogo ulisaidia mkoa huo kuwa wa pili kitaifa kwa viwanda vingi nyuma ya Dar es Salaam na kuzalisha ajira zaidi ya 14,000.
Hadi Desemba mwaka jana, NBS inaeleza kuwa Mara ilikuwa na viwanda 3,573 kati ya viwanda 50,656 vya Tanzania Bara sawa na asilimia 7.1 ikiwa na maana kuwa kwa kila viwanda 100 vilivyopo nchini, saba vinatoka mkoani humo. Mkoa wa Mara upo nyuma ya Dar es Salaam inayoongoza kwa kuwa na viwanda 15 kwa kila viwanda 100.
Hata hivyo, viwanda 3,377 sawa na asilimia 94.5 ya viwanda vyote mkoani humo vina uwezo wa kuajiri kati ya mtu mmoja hadi wanne.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hilo mkoani humo hususan halmashauri za Bunda Mjini na Musoma Manispaa, umebaini kuwa wajasiriamali wengi walihamasika kuanzisha viwanda vidogo miaka 10 iliyopita ili kuongeza vipato na kusaidia kukuza uchumi wakiwa na matumaini ya kukua kwa viwanda vya kati.
“Tulikuwa ni mafundi wa mtaani wa kushona viatu vikichanika, tuliona kazi ile haina maslahi tukaunda kikundi cha watu 11 mwaka 2010, tulijisajili na kuanza kiwanda kidogo kuongeza uzalishaji na kipato,” anasema Joseph Mwita (51), mwenyekiti wa kiwanda kidogo cha viatu cha Bunda Shoe Group kilichopo Bunda Mjini.
Kiwanda cha kina Mwita kinatengeneza viatu vya ngozi sawa kabisa na vinavyozalisha katika viwanda vikubwa nchini au kuingizwa toka nje. Tofauti na viwanda hivyo, kiwanda cha Bunda hakiwezi kutia nakshi ipasavyo kutokana na kukosa vifaa vya kisasa na mtaji.
Mbali na ukosefu wa vifaa, Bunda Shoe wanafanyia kazi zao ndani ya chumba kidogo cha wastani wa futi nane kwa 10 kiasi cha kushindwa kuhifadhi vyema viatu vilivyozalishwa.
Sehemu kubwa ya wajasiriamali wa viwanda hivyo vidogo wanaonekana kuviendesha kwa ajili ya kukabiliana na ukata na siyo kwa mipango ya muda mrefu ya kuwa viwanda vya kati.
Sensa ya viwanda inaonyesha kuwa mwaka 2013 kulikuwa na viwanda tisa vya kati mkoani Mara vyenye uwezo wa kuajiri watu kati ya 20-49 lakini hadi Desemba mwaka jana NBS ilionyesha viwanda vya aina hiyo vilikuwa 24 ikijumuisha viwanda vipya vilivyoanza ndani ya miaka hiyo mitatu.

Huu ni ukuaji dumavu
“Kasi ya ukuaji wa viwanda hivi hairidhishi ila hatukati tamaa kuwaelimisha wananchi njia za msingi za kuchochea ukuaji wa viwanda vyao ili viwe vya kati. Viwanda vidogo kamwe haviwezi kuwa mbadala wala kufidia hivi vikubwa vinavyofungwa,” anasema Meneja wa Maendeleo ya Viwanda Vidogo Vidogo (Sido) mkoa wa Mara, Frida Mungulu.
Anasema ukosefu wa ajira mkoani humo unahamasisha wananchi kujiajiri kwa kuendesha viwanda hivyo ili kujipatia kipato. Awali wananchi wa mkoa huo, anasema walikuwa wanategemea uvuvi, biashara ya mpakani na kilimo hususan pamba lakini shughuli hizo zimejaa ushindani au kuyumba hivyo viwanda vidogo vimegeuka tegemeo.
Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoa wa Mara, Boniphace Ndengo anasema mambo makubwa yaliyochochea viwanda vidogo mkoani humo ni uanzishwaji wa migodi ya dhahabu na kukua kwa uvuvi katika ziwa Victoria.
Viwanda hivyo licha ya kukabiliwa na udumavu, vinaajiri kundi kubwa la watu akiwamo Martha Evarist (23) aliyeajiriwa katika kiwanda kidogo cha sabuni na vipodozi cha Lubasu Soap Limited.
Martha, mama wa mtoto mmoja na wenziwe watano wameajiriwa kiwandani hapo na kujipatia kipato ambacho anasema awali ilikuwa ni vigumu kukipata.
“Natamani kiwanda chetu kiwe kikubwa, tuzalishe sabuni nzuri na nyingi kama vile vinavyozalisha Takasa na Pouwa. Napenda bidhaa zetu ziuzwe nje ya Mara ili hata kipato chetu kiongezeke,” anasema Martha.
Uwepo wa viwanda hivyo vinavyoweza kuajiri mtu mmoja hadi wanne, umesaidia kuzalisha zaidi ya ajira 7,300 sawa na asilimia 51 ya ajira zilizozalishwa ndani ya sekta hiyo kimkoa.
Licha ya mafanikio hayo, bado baadhi ya wajasiriamali wanaonekana kukata tamaa baada ya kushindwa kukua kwa muda mrefu wakidai wamekwamishwa na mazingira magumu ya biashara ukiwamo urasimu kutoka katika mamlaka za udhibiti kama vile Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).
James Mathayo, Mkurugenzi wa Kiwanda cha Mara Milk, kilichofungwa kutokana na kuelemewa na madeni na gharama kubwa za uzalishaji anasema kuna tozo nyingi za ukaguzi, majengo na bidhaa kutoka TFDA ikiwamo ya kusajili bidhaa kutokana na ujazo.
“Kwenye vipimo vya bidhaa unatakiwa utoe Sh500,000. Wakati wa kufungasha nao unatakiwa utoa fedha kutokana na ukubwa wa kifungashio Sh500,000,” anaeleza Mathayo ambaye kiwanda chake kilikuwa na uwezo wa kuajiri watu zaidi ya 80.
Anasema Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na TFDA wanafanya kazi zinazofanana hivyo ni bora taasisi hizo zikashirikiana ili kupunguza mzigo wa tozo ambazo anasema kuwa zinakatisha tamaa wajasiriamali.
TFD imeeleza kuwa haina nia ya kurudisha nyuma wawekezaji wa viwanda vidogo vidogo bali inahakikisha kila bidhaa ina ubora kulinda usalama na afya ya walaji.
Ofisa Mawasiliano wa TFDA, Gaudensia Simwanza anasema licha ya kuwapo mkakati wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati, hawawezi kuacha watu wazalishe bidhaa hatari kwa walaji.
“Tumekuwa tunawapa semina juu ya uzalishaji bora wa bidhaa ulio salama. Tunawaeleza kuwa jiko la kupikia ugali halifai kutengeneza bidhaa za biashara. Hivyo, wakifuata taratibu na kupatiwa usajili ni rahisi bidhaa kuuzwa hata kwenye ‘supermarkets’ (maduka makubwa),” anasema.
Kuhusu tozo kubwa, Simwanza anasema Serikali imepunguza tozo takriban 10 katika bajeti hii na kwamba nyingine hazizuiliki kwa kuwa kemikali zinazotumika kwenye vipimo ni ghali.
Licha ya mazingira magumu ya biashara ya kukosekana mitaji na mamlaka za udhibiti, ambacho ni kilio cha wengi, wamiliki wengine wa viwanda vidogo huenda wakafunga viwanda vyao siku zijazo kutokana na uhaba wa malighafi.
“Kadri siku zinavyoenda naona biashara inazidi kuwa ngumu sijui kama nitaendelea zaidi na kiwanda hiki. “Nasikitika tuna ziwa kubwa lakini viwanda vinafungwa,” anasema Fredrick Mtenga, mmliki wa kiwanda kidogo cha samaki.
Mtenga ambaye mahitaji yake ni kilogramu 500 kwa siku, kwa sasa anapata wastani wa kilogramu 20 na wakati mwingine hapati kabisa kutokana na kukithiri uvuvi haramu.
“Hali hii ikiendelea nitafunga kiwanda,” anasema Mtenga na kubainisha mpango wa kwenda kufuga kuku mkoani Morogoro.
Uchambuzi wa takwimu za sensa ya viwanda unaonyesha kuwa sehemu kubwa ya viwanda vidogo mkoani humo vilianzishwa baada ya mwaka 2005 baada ya rais mstaafu, Jakaya Kikwete kuingia madarakani.
Pamoja na changomoto hizo, viwanda vidogo vinaweza kukua na kuwa vya kati au vikubwa na kuchangia kiasi kikubwa cha maendeleo ya mkoa huo iwapo watabadili fikra na kuongeza ubora wa bidhaa zao.
“Viwanda vidogo ni kiashiria chema cha ukuaji wa viwanda ila iwapo kutakuwa na maboresho ya mazingira ya biashara kwa kuwa hata nchi zilizoendelea zilianza na viwanda vidogo ila maendeleo hayakutokea kwa siku moja,” anasema Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kuondoa Umaskini (Repoa), Dk Donald Mmari. Anasema wajasiriamali wa viwanda vidogo wanatakiwa kupatiwa elimu ya kutosha ya biashara, kurahisishiwa upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu na kuimarisha mnyororo wa thamani ili kusiwe na uhaba wa malighafi.
Katibu Tawala wa mkoa wa Mara, Adoh Mapunda anasema wanazidi kuboresha mazingira ya ukuaji wa viwanda vidogo kwa kuhakikisha kila halmashauri inatoa asilimia 10 ya mapato yake kuwakopesha wajasiriamali wanawake na vijana kuanzisha shughuli za uchumi vikiwamo viwanda vidogo.
“Tumekubaliana kwenye vikao kuwa kila halmashauri isichukue muda mrefu katika mchakato wa kumruhusu mwekezaji kuwekeza katika eneo husika ndani ya miezi mitatu ilimradi afuate taratibu,” anasema Mapunda.
Hata wakati baadhi ya wajasiriamali wakilalamikia mamlaka za udhibiti kama TFDA na TBS, Katibu Mkuu wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk Adelhelm Meru anasema kuwa ni vigumu kukwepa viwango vya ubora.
“Tulichofanya ni kuhakikisha TFDA na TBS zinashirikiana kwa karibu na wajasirimali hao kwa kuwapatia semina juu ya namna bora ya kuzalisha bidhaa zao kwa kufuata taratibu za viwango nchini,” anasema.
Dk Meru anasema Serikali inaijenga Tanzania ya viwanda hivyo itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji ikiwamo kusambaza nishati ya kutosha na kurahisisha taratibu za usajili wa biashara.