Mahakama yataka upelelezi wa kesi ya ‘Ndama mtoto wa ng’ombe’ ukamilishwe haraka

Muktasari:

Wakili wa Serikali, Leonard Challo ameiambia Mahakama kuwa kesi ilikuja kutajwa, lakini upelelezi wake bado haujakamilika na akaomba ipangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya kuangalia kama utakuwa umekamilika ama la.

Dar es Salaam. Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Victoria Nongwa ameuagiza upande wa mshtaka katika kesi ya  kughushi, kutakatisha fedha na  kujipatia dola za Marekani 540,390 kwa njia ya udanganyifu inayomkabili  Mfanyabiashara maarufu wa jijini Dar es Salaam, Ndama Shabani Hussein maarufu kama Pedeshee Ndama mtoto wa Ng'ombe(44) kukamilisha upelelezi haraka.

Wakili wa Serikali, Leonard Challo ameiambia Mahakama kuwa kesi ilikuja kutajwa, lakini upelelezi wake bado haujakamilika na akaomba ipangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya kuangalia kama utakuwa umekamilika ama la.

Baada ya kuelezwa hayo, Hakimu Nongwa ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 24,2017 na akauagiza upande wa mashtaka kuhakikisha upelelezi unakamilika haraka.

Mshtakiwa amepelekwa rumande kwa sababu moja kati ya mashtaka yanayomkabili la kutakatisha fedha halina dhamana.

Ndama anadaiwa kuwa Februari 20,2014 jijini Dar es Salaam,  alighushi nyaraka ya kibali cha kusafirisha madini na sampuli za madini kwa kusudi la kuonesha kuwa kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited iliruhusiwa kusafirisha maboxi manne ya dhahabu yenye kilogramu 207 yenye thamani ya Dola za Marekani 8,280,000.00 kwenda Australia  kwa kampuni ya Trade TJL DTYL Limited wakati akijua si kweli.