Mkuu wa mkoa akazia kaulimbiu ya viwanda
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego
Muktasari:
Katika kuhakikisha kuwa kaulimbiu hiyo inawaingia wawekezaji, Dendego amewataka watu walionunua viwanda serikalini kuvifufua badala ya kuvigeuza kuwa maeneo ya kutunzia korosho.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego amekazia kuhusu kaulimbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano ya uanzishaji na uimarishaji wa viwanda nchini.
Katika kuhakikisha kuwa kaulimbiu hiyo inawaingia wawekezaji, Dendego amewataka watu walionunua viwanda serikalini kuvifufua badala ya kuvigeuza kuwa maeneo ya kutunzia korosho.
Dendego ametoa maelekezo hayo wakati wa ufunguzi wa kikao cha wadau wa usimamizi wa msimu wa mauzo ya korosho kwa mikoa mitano.
Amesema kwamba kufufuliwa kwa viwanda hivyo kutasaidia kuongeza thamani ya zao hilo nchini kwa sababu
makubaliano ya Serikali na wamiliki hao yalikuwa ni kununua na kuviendeleza viwanda hivyo.
Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Hassan Jarufu amesema ufufuaji wa viwanda vya ubanguaji utawasaidia Watanzania wengi kunufaika kwa kupata ajira katika viwanda hivyo.
Amesema katika msimu wa mwaka 2016/17 kwa kushirikiana na wadau walidhibiti uuzwaji wa korosho nje ya mfumo wa stakabadhi ghalani maarufu kama Kangomba na kwamba, hivi sasa wanataka kuona wakulima wa zao hilo wananufaika zaidi kiuchumi.