Wanafunzi 58 wafutiwa matokeo kwa udanganyifu ikiwemo kutumia ChartGPT
Katibu Mtendaji Baraza la Mitihani Tanzania,Prof. Said Mohamed akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, kuhusu matokeo ya mtihani wa kidato cha sita na mitihani ya ualimu iliyofanyika mwezi Mei 2026.Picha na Michael Matemanga
Muktasari:
- Watahiniwa waliozuiwa matokeo ni 184 wa mtihani wa kidato cha sita (ACSEE), watano wa mtihani wa Stashahada ya Ualimu wa Elimu ya Msingi (DPEE) na mmoja wa Mtihani wa Stashahada ya Ualimu wa Sekondari (DSEE).
Dar es Salaam. Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) limezuia matokeo ya watahiniwa 190 mwaka 2026 kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo changamoto za kiafya, huku likifuta matokeo ya watahiniwa 58 waliobainika kufanya udanganyifu.
Aina ya udanganyifu huo ni kutumia 'notes' chumba cha mitihani, wengine kusaidiana majibu na baadhi kukamatwa na simu wakitumia Chart GPT kujibia mitihani.
Watahiniwa waliozuiwa matokeo ni 184 wa mtihani wa kidato cha sita (ACSEE), watano wa mtihani wa Stashahada ya Ualimu wa Elimu ya Msingi (DPEE) na mmoja wa Mtihani wa Stashahada ya Ualimu wa Sekondari (DSEE).
Taarifa hiyo ya matokeo ya mitihani ya kidato cha sita na ualimu kwa Mei 2026 imetolewa na Katibu Mtendaji wa Necta, Profesa Said Mohamed akisema leo Jumatatu, Julai 6, 2026 jijini Dar es Salaam akisema watahiniwa waliozuiwa watapewa fursa ya kurudia kufanya mtihani mwaka 2027 kwa mujibu wa Kifungu cha 32(1) cha kanuni za Mitihani.
Aidha, amesema baraza hilo limefuta matokeo ya watahiniwa 58 baada ya kubainika kujihusisha na vitendo vya udanganyifu katika mitihani.
"Kati ya hao, watahiniwa 44 ni wa Mtihani wa Kidato cha Sita, wakiwemo 36 wa shule na wanane wa kujitegemea, huku watahiniwa 14 wakiwa wa Mtihani wa Stashahada ya Ualimu wa Elimu ya Msingi (DPEE)," amesema.
Profesa Mohamed amesema hatua hiyo imechukuliwa kwa mujibu wa kifungu cha 5(2)(i) na (j) cha Sheria ya Baraza la Mitihani, Sura ya 107, kikisomwa pamoja na Kifungu cha 30(2)(b) cha Kanuni za Mitihani za mwaka 2016.
Katika hatua nyingine, amesema Necta imeifungia kituo cha mitihani cha P5584 Excellency Open School kilichopo Mkoa wa Manyara baada ya kubainika kukiuka miongozo ya uendeshaji wa Mitihani ya Taifa.
Kkituo hicho kimefungiwa kwa mujibu wa Kifungu cha 4(8) cha Kanuni za Mitihani za mwaka 2016 na hakitaruhusiwa kuendesha Mitihani ya Taifa hadi Baraza hilo litakapojiridhisha kuwa kina mazingira salama na kinakidhi masharti ya uendeshaji wa mitihani.
Aidha, amesema tahasusi za lugha, sayansi jamii na biashara na uchumi watahiniwa wake wamepata ufaulu wa Daraja la kwanza hadi la tatu kwa asilimia kati ya 95.25 hadi 97.17.
Amesema katika tahasusi za sayansi asilia watahiniwa waliofaulu madaraja hayo ni asilimia 77.68 na katika tahasusi za ualimu masomo ya sayansi na biashara watahiniwa wengi asilimia 72.75 wamepata ufaulu wa Daraja la tatu.
"Idadi kubwa ya watahiniwa waliopata daraja la I-II inapatikana katika tahasusi za Sayansi Jamii zenye jumla ya watahiniwa 40,721 ikifuatiwa na tahasusi za Sayansi Asilia zenye watahiniwa 38,098 na tahasusi za Biashara na Uchumi zina watahiniwa 16,830 waliopata madaraja hayo," amesema.