Wagonjwa 500 wapasuliwa vichwa Zanzibar

Muktasari:

Dk Shein alisema hayo alipozungumza na ujumbe wa wataalamu wa upasuaji wa kichwa na uti wa mgongo kwa nchi za Bara la Afrika waliofika Ikulu mjini Zanzibar.

Zanzibar. Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema visiwa hivyo vimepata mafanikio katika sekta ya afya baada ya kufanikiwa kuwafanyia upasuaji wagonjwa 500 wa maradhi ya kichwa na uti wa mgongo.

Dk Shein alisema hayo alipozungumza na ujumbe wa wataalamu wa upasuaji wa kichwa na uti wa mgongo kwa nchi za Bara la Afrika waliofika Ikulu mjini Zanzibar.

Alisema wagonjwa hao kutoka Unguja na Pemba wamefanyiwa upasuaji huo wakiwamo watoto.

Alisema mafanikio hayo yanatokana na juhudi za wahisani wa maendeleo kutoka nchi rafiki waliofika kusaidia sekta ya afya na hasa sehemu ya upasuaji.

Dk Shein alisema licha ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuokoa kiasi kikubwa cha fedha zilizokuwa zikitumika kwa ajili ya kuwatibu wagonjwa wa maradhi hayo nje ya nchi, faraja iliyopo ni kuona huduma hiyo muhimu inatolewa nchini.

Alisema juhudi zilichukuliwa na Serikali ya Zanzibar katika kuhakikisha inanunua vifaa muhimu na vya kisasa ikiwamo mashine ya MRI na za kusafisha damu kwa wagonjwa wenye matatizo ya figo.

Timu ya wataalamu iliongozwa na rais wa taasisi ya maendeleo ya elimu ya mishipa ya fahamu, uti wa mgongo na vichwa (NED), Dk Hosea Piquer.