Rais Magufuli aitaka Israel kufungua ofisi ya ubalozi

Rais John Magufuli 

Muktasari:

Pia, ameeleza kufurahishwa na ujio wa ndege iliyobeba watalii 200 na wawekezaji kutoka Israel.

Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikifungua ubalozi wake nchini Israel, Rais John Magufuli ametoa wito kwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kufungua ubalozi wake hapa nchini.

Pia, ameeleza kufurahishwa na ujio wa ndege iliyobeba watalii 200 na wawekezaji kutoka Israel.

Rais Magufuli alisema hayo jana alipokutana na balozi wa Israel hapa nchini, Yahel Vilan Ikulu jijini Dar es Salaam. Rais alimhakikishia balozi huyo kuwa Tanzania imedhamiria kuimarisha na kukuza uhusiano na ushirikiano wake na taifa hilo la mashariki ya mbali, hasa katika masuala ya uwekezaji, biashara, utalii na uboreshaji wa huduma za kijamii.

Mwaka jana Israel ilifungua ofisi ndogo ya ubalozi nchini.

Katika taarifa iliyotolewa naKurugenzi ya Mawasilino ya Rais, Ikulu, Rais Magufuli amesema ili kufanikisha dhamira hiyo Tanzania imefungua ubalozi nchini Israel na amemuomba balozi huyo kupeleka ujumbe kwa Netanyau kuhusu nchi hiyo kufungua ofisi za ubalozi nchini.

“Naamini uhusiano na ushirikiano wetu utaongeza manufaa zaidi kwa nchi zetu na watu wake. Nimefurahishwa sana na taarifa kuwa watalii wataanza kuja kwa ndege moja kwa moja kutoka Tel Aviv, Israel na hivi karibuni ndege yenye watalii zaidi ya 200 itakuja nchini kwetu. Nawakaribisha sana watalii na wawekezaji kutoka Israel,” alisema Rais Magufuli.

Balozi Vilan aliahidi kuwa Israel itajenga jengo la wagonjwa wenye kuhitaji uangalizi wa maalumu (ICU) katika Hospitali ya Benjamin Mkapa mkoani Dodoma mwishoni mwa mwaka huu.

Alisema Israel itaendelea kushirikiana na Tanzania kwa kuunga mkono juhudi za maendeleo, ikiwamo ujenzi wa viwanda, kilimo na kuimarisha huduma za matibabu kwa wananchi.

Wakati huohuo, Rais Magufuli amemshukuru balozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Roeland Van de Geer kwa msaada wa Euro 205 milioni (takribani Sh500 bilioni) kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za maendeleo nchini kwa kipindi cha miaka minne ijayo.

Alisema kutolewa kwa fedha hizo kumethibitisha uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya na kwamba pamoja na kutoa fedha hizo umoja huo unatarajia kutoa Euro 1.2 bilioni nyingine kwa ajili ya kuendeleza viwanda, kilimo na uzalishaji wa nishati.

“Nimefurahi sana kwamba uhusiano na ushirikiano wetu unajikita kushughulikia mambo ya msingi kwa Watanzania. Nakuhakikishia kuwa fedha mnazotoa zitatumika vizuri na zitatoa mchango mkubwa katika maendeleo yetu,” alisema Rais Magufuli.

Balozi Roeland Van de Geer alimpongeza Rais kwa uongozi wake na dhamira yake ya kujenga uchumi na kusimamia utawala bora, ikiwamo mapambano dhidi ya rushwa, huku akiahidi kuwa nchi wanachama wa umoja huo zitaendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano wake na Tanzania.