Friday, April 14, 2017

‘Serikali haina uhasama na wafanyabiashara’

wenyekiti wa Umoja wa Maofisa Watendaji Wakuu

wenyekiti wa Umoja wa Maofisa Watendaji Wakuu wa Kampuni Binafsi nchini (CEOrt), Ali Mufuruki. 

By Elizabeth Edward, Mwananchi eedward@wananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Umoja wa Maofisa Watendaji Wakuu wa Kampuni Binafsi nchini (CEOrt), Ali Mufuruki amesema Serikali imewahakikishia wafanyabiashara kuwa haina matatizo nao.

Akizungumzia mkutano uliowakutanisha wadau wa sekta binafsi na Serikali juzi, Mufuruki alisema wafanyabiashara wamehakikishiwa kuwa wana mchango mkubwa kwenye uchumi wa Taifa na kwamba Serikali haiwezi kujenga uchumi bila kuwahusisha.

“Tulikuwa na mkutano na Serikali nasi kama sekta binafsi tukatoa maoni yetu tukawaambia dukuduku tulizonazo, tukionyesha wasiwasi wetu wa kuwapo kwa uhasama ambao unaonekana kuanza kujitokeza kati yetu na Serikali, lakini wametuhakikishia kuwa hali haiko hivyo.

“Tumehakikishiwa pia kuwa Serikali inaamini kuwa haiwezi kujenga uchumi wa Taifa letu bila ushirika na sekta binafsi na inapenda kufanya biashara na wafanyabiashara,” alisema Mufuruki.

Katika hatua nyingine Mufuruki alisema Ceort itaendelea kuwa mstari wa mbele kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kupunguza hatari inayoweza kusababishwa na shughuli mbalimbali za uzalishaji.

Alisema bado zipo changamoto mbalimbali zinazoendelea kuwa kikwazo katika jitihada za kukuza uchumi wa Tanzania, mojawapo ikiwa ni uharibifu wa mazingira.

Alisema Ceort kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Utunzaji wa Mazingira (IUCN) wanaangalia namna gani sekta binafsi inavyoweza kutoa mchango katika utunzaji wa mazingira.

“Tunashirikiana na wadau hawa wa mazingira kuangalia namna gani tunavyoweza kuweka mchango wetu kwenye suala zima la utunzaji wa mazingira na kuokoa sehemu ambazo tayari yameshaathiriwa na kutokana na mabadiliko ya tabia nchi au uharibifu unaofanywa na binadamu,” alisema.

Mwakilishi wa IUCN, Michael Kwameh aliipongeza Ceort kwa kuchukua hatua na kushiriki kikamilifu katika kutatua changamoto ya uharibifu wa mazingira nchini.

“Biashara zinatakiwa kufanywa katika mazingira mazuri hivyo ni jukumu la kila mmoja kutunza mazingira hayo. Hili siyo jukumu la Serikali peke yake ndiyo sababu nawapongeza Ceort kwa kuonyesha mfano na kulipa kipaumbele suala la mazingira,” alisema.

-->