Dodoma kuunda kikosi kazi kubadili hati miliki zilizotolewa na CDA

Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi

Muktasari:

  • Mei 15, mwaka huu Rais John Magufuli alivunja CDA pamoja na bodi yake.

Dodoma. Manispaa ya Dodoma imesema itaunda kikosi kazi kitakachoshirikiana na kamishna wa ardhi ili waweze kubadili hati miliki za viwanja 56,000 zilizogawawiwa na iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) kutoka umiliki wa miaka 33 kwenda miaka 99 kwa mujibu wa sheria.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi ametoa kauli hiyo leo , Jumanne mjini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na hatua mbalimbali zilizofikiwa katika kuhakikisha kuwa amri ya Rais John Magufuli inatekelezwa katika kuhamishia kazi zilizokuwa zinafanywa na CDA kwa manispaa hiyo.

Kunambi amesema kuwa hati miliki hizo 56,000 ni zile zilizotolewa na CDA kwa kipindi cha miaka 30 kuanzia mwaka 1987 hadi mwaka 2017.

Amesema jukumu la kikosi kazi hicho litaanza mara moja baada ya kamishna wa ardhi kukutana na uongozi wa manispaa ambaye alikuwa anatarajiwa kuwasili leo mjini Dodoma kwa ajili ya kazi hiyo.

“Tunatakiwa kuzibadilisha hati miliki hizo kutoka miaka 33 iliyokuwepo hapo awali kwenda miaka 99 kwa kipindi kifupi sana ili kila mtu awe na hati miliki ya ardhi yenye miaka 99,” amesema Kunambi.