Lissu asema mawakili waliokwenda mahakamani hawana mshikamano

Baadhi ya mawakili wakiwa na wateja wao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana. Picha na Omari Fungo

Dar/mikoani. Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu amesema mawakili walioenda mahakamani jana hawana mshikamano.

Jana ilikuwa siku ya kwanza kwa mawakili kote nchini kususia shughuli za mahakama kwa siku mbili kuonyesha kutokubaliana na kulipuliwa kwa ofisi ya mawakili ya Immma Advocates iliyopo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Lakini lakini utekelezaji wake haukuwa kamilifu kutokana na baadhi kwenda mahakamani kuendelea na shughuli zao na wengine kutii maelekezo ya TLS.

“Waacheni mawakili hao waendelee na kazi kwa kuwa hatujui kesho nao watapatwa na majanga gani,” alisema Lissu.

Miongoni mwa waliofika mahakamani jana ni pamoja na wakili wa kampuni iliyolipuliwa ya Imma Advocates, Gaspar Nyika ambaye alienda Mahakama Kuu kwa ajili ya kesi ya mteja wake.

Akizungumza na Mwananchi, Nyika alisema utekelezaji wa maagizo ya TLS unategemeana na mazingira na kwamba kwa namna moja ni vigumu kutekeleza.

“Sisi tumeingia mkataba na wateja, sasa usipokwenda mahakamani kumwakilisha katika kesi yake unakuwa umevunja mkataba. Labda kama mteja atakubali, lakini kama hajakubali hilo linakuwa gumu kulitekeleza,” alisema Wakili Nyika.

Nyika alisema suala hilo lilihitaji pia uungwaji mkono wa mahakama na kwamba kutokwenda mahakamani itakuwa ni kwenda kinyume cha agizo la Kaimu Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma aliyesema wakili ambaye hatakwenda mahakamani sheria itachukua mkono wake.

Katika mikoa mbalimbali kama Kilimanjaro, kiongozi wa TLS wa mkoa, Elikunda Kipoko alisema shambulio lililofanywa ofisi za Immma ni dhidi ya Watanzania na wapenda amani wote, hivyo wameamua kugoma.

Kipoko alisema Immma ni ofisi inayotoa huduma ndani ya Tanzania kama zilivyo nyingine au taasisi nyingine, hivyo wote wenye ofisi na wanaopata huduma kwenye ofisi hizo ni shambulio linalowagusa.

Alisema ni wa hiyari na ni kama vile ilivyo mtu kutolazimishwa kuomboleza.

Kipoko aliongeza kuwa TLS imeamua kuujulisha umma kuwa hawastahili kukaa kimya kama uvunjivu wa sheria unatokea.

“Watu wanajiuliza, mbona TLS haikuchukua hatua kiasi hiki katika matukio yaliyotangulia? Jibu ni kwamba haimaanishi tunaendelea kukaa kimya, tunaendelea kuitafuta haki na amani,” alisema Kipoko.

Hata hivyo, wakati Kipoko akisema hayo, Msajili wa Mahakama Kuu, Bernard Mpepo amesema hakuna mgomo wowote unaoendelea mkoani Kilimanjaro.

“Ni kwamba mawakili wote wameingia mahakamani tangu asubuhi na wanaendelea na majukumu yao kama kawaida,” alisema.

Mkoani Arusha, mgomo ulianza kwa kusuasua, lakini baadaye wengi wakaonekana kuendelea na kazi za kutetea wateja wao.

Tangu asubuhi, mawakili walikuwa katika makundi makundi kwenye viwanja vya Mahakamaa Kuu na baadaye baadhi waliamua kuendelea kutetea wateja.

Mwenyekiti wa TLS wa Arusha, Elibariki Maeda alisema mgawanyiko huo wa mawakili umetokana na kuchelewa kutolewa taarifa kwa ngazi za juu za mahakama.

Alisema mkoa unaunga mkono tamko la Rais wa TLS.

“Kwa sasa tumeanza kuona jitihada za polisi kuchunguza, lakini tunataka watuhumiwa wakamatwe,” alisema.

Mkoani Mbeya, mawakili waligawanyika. Katika Mahakama Kuu, baadhi walifika kuendelea na kazi wengine hawakufika na hivyo kesi za wateja wao kuendeshwa upande mmoja, jambo lililosababisha baadhi kuahirishwa.

Wakizungumza na nje ya Mahakama Kuu jana, baadhi ya mawakili walidai kuwa wameingia mkataba na wateja wao na kwamba wanafanya kazi chini ya mahakama; wanapewa leseni za uwakili na Jaji Mkuu na kwamba kugoma ni kuingilia kazi ya uchunguzi inayofanywa na vyombo vya dola.

Mawakili wa TSK Law Chambers, Dk Tasco Luambano na Kamru Habibu walisema wanafanya kazi kwa maelekezo ya wateja wao na walifika mahakamani hapo jana asubuhi kwa ajili hiyo na kama wasingefika mteja wao angeathirika wakati alishalipia gharama.

“Hivyo basi ili kuepuka madhara yanayoweza kumpata mteja wetu, tumeona ni busara zaidi kutetea masilahi ya mteja wetu na sisi pia ambao tumelipwa,” alisema Dk Luambano.

Wakili Ladislaus Lweikaza alitoa hoja kama hiyo akisema wanafanya kazi chini ya mahakama, hivyo ikitokea kesi ikafutwa au ikaamriwa kwa namna yoyote kwa sababu ya wakili kutofika mahakamani, wanaweza kuchukuliwa hatua kali ikiwamo ya kufutiwa leseni.

Ofisi za Immma zilishambuliwa usiku wa kuamkia Jumamosi na tangu wakati huo kumekuwa na taarifa tata kuhusu mlipuko huo, baadhi zikisema ni wa bomu na nyingine zikisema ni wa bomu la petroli.