Star Media yatozwa Sh100 milioni kwa kutoza fedha chaneli za bure

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba

Mwanza. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeitoza faini ya Sh100 milioni kampuni ya Star Media kwa kuwatoza fedha watazamaji wa chaneli zinazotakiwa kuonekana bila kulipiwa kupitia king’amuzi cha Star Times.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza jana, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba alisema kitendo hicho ni kinyume cha kanuni ya 14(2) (a) ya kanuni za Digital and Broadicasting Networks za mwaka 2011.

“TCRA inaendelea kufuatilia kuhakikisha kuwa ving’amuzi vya Star Times, Continental, Digitek na Ting vinaendelea kuonyesha chaneli zote za kitaifa za FTA (Free to Air) bure kwa mujibu wa sheria,” alisema Kilaba.

Chaneli zinazotakiwa kuonekana bila kulipiwa ni TBC1, ITV, EATV, Channel Ten, Star TV na Clouds TV. Kampuni hiyo imetozwa faini kuanzia Desemba 22 na inatakiwa kuwa imelipa kabla ya Januari 30.

Akizungumzia uamuzi huo, mkazi wa jijini Mwanza, Pius Rugonzibwa alipongeza akisema wamekuwa wakipata usumbufu kwa kukatiwa huduma.

Gharama mpya za mtandao

Mbali ya adhabu hiyo kwa Star Media, Kilaba pia alitangaza viwango vipya vya gharama za mwingiliano baina ya mitandao inayotoa huduma za mawasiliano ya simu nchini vitakavyoanza kutumika Januari Mosi baada ya vinavyotumika sasa kufikia kikomo Desemba 31.

Alisema kampuni za simu zimekuwa na kigugumizi kukubaliana kuhusu viwango hivyo na kuingia mikataba ya mwingiliano kwa sababu ya masilahi ya kibiashara hivyo TCRA ililazimika kuingilia kati na kuvipanga kwa kufuata utaratibu kama ilivyoainishwa katika sheria namba 12 ya kuanzishwa kwake mwaka 2003.

Alisema kampuni hizo hulipana kufidia ya gharama ya kupokea simu inayotoka mtandao mwingine na kuifikisha kwa mteja aliye ndani ya mtandao unaopigwa.

Kilaba alisema TCRA iliweka viwango kwa mtiririko wa kipindi cha miaka mitano kinachoishia Desemba 31.

Gharama za mwingiliano zitakazotozwa kwa dakika na mwaka kwenye mabano ni Sh15.60 (Januari Mosi, 2018), Sh10.40 (2019), Sh5.20 (2020), Sh2.60 (2021) na Sh2.00 (2022).

Alisema viwango hivyo vimepungua kulinganisha na miaka mitano iliyopita ambayo gharama zake za mwingiliano zilizokuwa zikitozwa kwa dakika na mwaka wake kwenye mabano ilikuwa Sh34.92 (2013), Sh32.40 (2014), 30.58 (2015), Sh28.57 (2016) na Sh26.96 (2017).

“Kupungua kwa gharama hizi kutawezesha na kuongeza ufanisi katika shughuli za sekta zingine kiuchumi na kijamii, pia kutaongeza mapato ya watoa huduma na Serikali kutokana na ongezeko la matumizi ya huduma za mawasiliano,” alisema.

Alisema kwa sasa simu za mezani ni 127,976 na watumiaji wa simu za kiganjani imeongezeka kutoka laini 2,963,737 mwaka 2005 hadi kufikia laini 40,002,364, Septemba.

Alisema mpaka kufikia Septemba, watumiaji wa huduma wamefikia 21,611,855.