Zitto apinga sheria iliyotumiwa na polisi kuzuia mkutano wake Kigoma

Muktasari:

Mkutano huo umezuiwa na mkuu wa polisi wa Wilaya ya Kigoma, SP Mayunga ambaye katika barua aliyoiandikia ACT-Wazalendo amesema chama hicho hakikufuata matakwa ya sheria inayotaka kutoa taarifa saa 48 kabla ya mkutano.

Dar es Salaam. Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amelalamikia kitendo cha polisi kuzuia mkutano wake, akisema ni kinyume na Sheria ya Bunge namba 4(1) inayotoa uhuru kwa wabunge kufanya mikutano.

Mkutano huo umezuiwa na mkuu wa polisi wa Wilaya ya Kigoma, SP Mayunga ambaye katika barua aliyoiandikia ACT-Wazalendo amesema chama hicho hakikufuata matakwa ya sheria inayotaka kutoa taarifa saa 48 kabla ya mkutano.

“Kwa muktadha wa kifungu cha 43(1), Sura ya 322 marejeo ya mwaka 2002, taarifa yako haijakidhi matakwa ya kutoa taarifa saa 48 kabla na pia haijaainisha muda wa kuanza na kumaliza kwa mkutano,” inasema barua hiyo ya polisi.

“Kwa mamlaka niliyopewa narejea kifungu cha sheria 43(1), Sura ya 322 marejeo ya mwaka 2002 nakuzuia kufanya mkutano huo.”

Baada ya kupokea barua hiyo, Zitto ambaye pia ni kiongozi wa ACT-Wazalendo aliandika taarifa yake na kuituma katika mitandao ya Twitter na Facebook, akisema Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge inalazimisha mbunge kufanya mkutano kwenye jimbo lake bila vikwazo.

“Mimi sitaki kuwapa polisi sifa ya kupambana nasi. Tumeahirisha mkutano mpaka siku ya Jumamosi, lakini tumewaandikia barua rasmi kuwa sheria waliyonukuu si sheria halali na haihusiani na mikutano ya mbunge kwenye jimbo lake la uchaguzi. Sheria wanayopaswa kunukuu ni sheria namba 3 ya mwaka 1988 kifungu cha 4(1),” alisema Zitto.

Pia alisema atamwandikia barua Spika Job Ndugai kuhusu suala hilo ili lisifanyike kwa mbunge mwingine.

Polisi wilayani Kigoma walisema walipokea barua za chama hicho Januari 15 iliyofika saa 9:50 alasiri na nyingine ya Januari 16 iliyowafikia saa 3:07 asubuhi.

Kitendo hicho pia kimepingwa na mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema alisema demokrasia inaendelea kupita katika majaribu makubwa.

“Ninalaani tabia ya kuzuia wabunge kufanya mikutano jimboni. Hivi karibuni tukio kama hilo lilitokea Tarime ambako (mbunge wa Tarime kwa tiketi ya Chadema, Esther) Matiko alizuiwa kufanya mkutano na sasa Zitto amezuiwa kufanya mkutano jimboni kwake,” alisema Lema.