Serikali yaikomalia mikataba vyama vya ushirika

Muktasari:

Mali za ushirika zilizoshikiliwa bila kufuata utaratibu nazo kuchunguzwa.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea kuchunguza mikataba mibovu ndani ya vyama vya ushirika, zikiwamo mali zinazoshikiliwa kinyume na utaratibu.

Akizungumza bungeni leo Februari 9, 2018 wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 10 wa Bunge la 11, Majaliwa amevitaja vyama vinavyofanyiwa uchunguzi kuwa ni Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza (NCU), Chama Kikuu cha Ushirika cha Shinyanga (Shirecu), Chama Kikuu cha Ushirika cha Kagera (KCU), Chama Kikuu cha Ushirika cha Kilimanjaro (KNCU).

Pia, amesema Serikali inachunguza kushikiliwa kwa mali za ushirika bila kufuata utaratibu, “Serikali imeagiza mali za NCU na Shirecu zirudishwe kwenye vyama husika na watuhumiwa wachukuliwe hatua za kisheria.”

Alizitaja mali hizo za NCU ni pamoja na jengo la Nyanza Cooperative Union (1984) Ltd maarufu kwa jina la “Transport House” au KAUMA House, lililopo katika kiwanja namba 242, Kitalu T, Mtaa wa Station Road.

Nyingine ni kiwanda cha kusindika mafuta cha New Era Oil Mill,

kilichopo katika eneo la Igogo, jengo na viwanja vya Ashock Industries vilivyopo eneo la viwanda Igogo.

Majengo mengine yaliyochukuliwa ni kiwanda cha mkonge na Dengu kilichopo Igogo, kiwanja namba 41 na 79, jengo lililopo katika kiwanja kilichopo Isamilo namba 80, Kitalu “D” na jengo lililopo katika kiwanja kilichopo Isamilo namba 110, kitalu “D”.

Mali nyingine ni ghala moja katika kiwanja namba 104, Kitalu “A” kilichopo eneo la Igogo, jengo moja lililopo mjini Geita katika kiwanja namba 8 kitalu “K” ,jengo moja lililopo mjini Geita, katika kiwanja namba 24, Kitalu “K” na kiwanja kilichopo Isamilo katika kiwanja namba 89 Kitalu “D”.

Kwa upande wa Shirecu ni ghala lililopo Kurasini, Dar es Salaam na nyumba ya ghorofa tatu iliyopo kiwanja namba 1001 “BB” Ilala, Dar es Salaam.

“Serikali itaendelea kuviamsha vyama vya ushirika vya msingi na vyama vikuu vilivyosinzia katika mikoa yote ili kujenga ushirika imara,”amesema.

Amesema mali tisa za NCU zimepatikana na zimerudi kwenye ushirika huo wakati mali moja bado iko kwenye hatua ya uchunguzi.

Amebainisha kuwa kwa upande wa Shirecu, mali zote zimepatikana na ziko kwenye hatua ya makabidhiano.

“Juhudi na hatua hizo zinazochukuliwa na Serikali, zinalenga kuongeza imani, hamasa na uzalishaji wa mazao na kusimamia masoko yake, na hivyo, kuinua kipato cha wakulima sambamba na kuwapatia fursa ya kujiajiri katika sekta ya kilimo,”amesema.