Vitabu vya mchungaji KKKT vyakusanywa

Muktasari:

  • Vitabu hivyo vyenye kurasa 98 vinaondolewa kwenye mzunguko ikiwa ni agizo la Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Moshi, ambayo ilimkamata na kumhoji mchungaji huyo wiki iliyopita.

Usharika wa Karanga wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), umeanza kazi ya kukusanya vitabu vya taarifa ya mchungaji kiongozi wao, Fred Njama.

Vitabu hivyo vyenye kurasa 98 vinaondolewa kwenye mzunguko ikiwa ni agizo la Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Moshi, ambayo ilimkamata na kumhoji mchungaji huyo wiki iliyopita.

Katika vitabu hivyo, ipo hotuba ya Mchungaji Njama iliyotaja mambo sita yanayolitafuna taifa kwa sasa, ambayo kamati hiyo ya ulinzi na usalama inadai yana uchochezi wa kisiasa.

Mambo aliyoyataja mchungaji huyo ni tangazo la elimu bure lilivyoporomosha elimu, ughali wa matibabu, kuongezeka kwa umasikini, tatizo la ajira na kutolipwa mafao kwa wastaafu. Pia Mchungaji Njama, ambaye ni mkuu wa pili wa Jimbo la Kilimanjaro Kati katika dayosisi hiyo, alizungumzia kuminywa kwa uhuru wa haki za binadamu, vyombo vya habari na siasa.

Haijafahamika ni vitabu vingapi vinatakiwa kukusanywa, lakini jana Mwananchi lilishuhudia kazi ya kukusanya vitabu hivyo ikiendelea katika usharika huo na ilielezwa kazi hiyo ilianza juzi.

Mmoja wa watumishi wa usharika huo, ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema ni kweli vitabu vimeanza kurudishwa lakini akasema hawezi kutaja idadi na ni nani waliorudisha.

Mwandishi wa Mwananchi (jina linahifadhiwa) ni miongoni mwa waliorudisha vitabu hivyo (pichani).

Mchungaji Njama mwenyewe alipotafutwa hakupatikana kuzungumzia suala hilo, lakini katibu mkuu wa Dayosi ya Kaskazini, Arther Shoo alidai yeye hana taarifa vitabu hivyo vinapelekwa wapi.

Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Hamis Issah alikaririwa na Mwananchi akisema suala la mchungaji huyo lilikuwa limeshughulikiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya.

Hata hivyo, mwenyekiti wa kamati hiyo, Kippi Warioba alipotafutwa hivi karibuni alisema hawezi kulizungumzia kupitia kwenye simu na kutaka mwandishi aende ofisini, ambako hata hivyo hakuwepo.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira alipotafutwa kuzungumzia hilo alisema: “Bado sijapewa taarifa rasmi mpaka mkuu wa wilaya anipe hizo taarifa hivyo kwa sasa siwezi kulizungumzia.”

Mghwira alisema suala la Mchungaji Njama aliliacha likiwa kwenye hatua ya kwanza na kama kuna kinachoendelea bado hajafahamishwa rasmi.

Jumapili iliyopita katika ibada ya kwanza, Mchungaji Njama alieleza kwa kirefu namna alivyoitwa na kamati hiyo na kuhojiwa kuhusiana na hotuba yake hiyo ambayo inadaiwa kutoifurahisha Serikali.

Mchungaji Njama alidai baada ya kuhojiwa, wajumbe wa kamati hiyo walitaka kupelekwa alikochapishia vitabu hivyo na wakiwa na polisi wenye silaha walifika kiwandani na kuchukua kitabu kimoja

“Kabla ya kufanyika kwa mkutano mkuu, taarifa yetu ilipelekwa katika ofisi ya Dayosisi na kuhakikiwa na baadaye ikarudishwa baada ya kuonekana ni sahihi,” alisema Mchungaji Njama. Kukamatwa kwa mchungaji huyo kumeibua hisia miongoni mwa waumini na jamii na kwenye mitandao.

Wakili wa kujitegemea wa jijini Dar es Salaam, Frank Mushi alisema kukamata watu wanaotumia haki yao ya kikatiba kutoa maoni yao kunaichafua taswira nzuri ya Tanzania kimataifa.

“Katiba inamruhusu na inampa kila mtu kushiriki katika shughuli za Serikali yake. Ikitokea alichokisema si ukweli anapaswa kuelezwa ukweli ni upi si kukamatwa”, alisema Mushi.

“Serikali itawajibika kwa wananchi, sasa kama mwananchi anasema kuna shida Serikali inatakiwa iseme hiki anachokisema sio sawa ila ukweli ni huu. Kutofautiana kimtizamo sio kosa” alisisitiza.

Wakili huyo alitolea mfano wa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete aliyewahi kusema mtu akisema Serikali haijafanya chochote, Serikali inapaswa kuwaonyesha barabara, shule na hospitali.