Mwanamke akutwa amefariki dunia gesti Chalinze

Muktasari:

Mwili umekutwa kitandani bila jeraha lolote

Felister Mtinga, anayekadiriwa kuwa na kati ya miaka 30 hadi 36, amekutwa amekufa katika nyumba ya kulala wageni iliyopo Chalinze Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.

Mwili wa marehemu umekutwa kitandani bila jeraha lolote.

Akizungumza leo Jumanne Machi 27, 2018 kamanda wa polisi mkoani Pwani, Jonathan Shana amesema tukio hilo limebainika Machi 26, 2018 saa 4:00 asubuhi wakati wahudumu wa gesti hiyo walipokuwa wakifanya usafi.

"Wahudumu wa nyumba hiyo ya kulala wageni wamesema walimpokea juzi akiwa peke yake wakampatia chumba, lakini jana hawakumuona akitoka baada ya kugonga mlango wake ukawa umefungwa kwa ndani,” amesema.

Amesema wahudumu hao baada ya kuona hali hiyo, wamelazimika kutoa taarifa polisi ambao wamefika eneo hilo na kuvunja mlango hivyo kukuta mwili ukiwa kitandani.

"Uchunguzi wa awali umefanyika na kubaini kutokuwa na majeraha. Mwili umehifadhiwa Hospitali ya Rufaa  Mkoa wa Pwani  hivyo tunawaomba watu ambao watakuwa hawamuoni ndugu yao wajitokeze ili kutambua  mwili huo kwa taratibu nyingine,” amesema.