Mahakama yazuia kwa muda matumizi ya kanuni za mtandao

Muktasari:

Taasisi tano ikiwamo Tef ziliwasilisha maombi hayo mahakamani na kesi hiyo imepangwa kusikilizwa Mei 10.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara leo Mei 4, 2018 imetoa zuio la muda linalozuia matumizi ya Kanuni za Maudhui ya Kimtandao ambazo matumizi yake yalipaswa kuanza rasmi Mei 5, 2018.

 

Akizungumza na MCL Digital leo, Katibu wa Jukwaa la Wahariri (Tef), Neville Meena amesema zuio hilo limetolewa leo baada ya taasisi sita, ikiwemo Tef, kuwasilisha mahakamani maombi ya kuzia matumizi ya kanuni hizo April 30, 2018.

 

Taasisi zilizowasilisha maombi hayo mahakamani ni Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (LHRC), Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRD), Baraza la Habari Tanzania (MCT), Jamii Media, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) na Tef.

 

Taasisi hizo katika kesi ya msingi ya mapatio ya kanuni hizo, zimewashitaki Waziri wa Habari, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

 

Katika maombi ya msingi taasisi hizo zinaiomba Mahakama Kuu kufanya mapitio ya kanuni hizo kwa kigezo kwamba; Waziri ametumia nguvu ya kisheria nje ya mamlaka yake, zinakiuka kanuni za usawa, kanuni hizo zinapingana na haki ya kujieleza, haki ya kusikilizwa pamoja na haki ya usiri.

 

Kesi ya msingi imepangwa kusikilizwa Mei 10, 2018.